NA KASSIM ABDI, OMPR
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na waandishi wa habari kwa kundoa vikwazo wanavyokabiliana navyo katika upatikanaji wa taarifa kutoka taasisi za serikali.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleima Abdulla, alieleza hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani yaliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss abdulwakili, Kikwajuni jijini Zanzibar.
Alieleza kuwa serikali inathamini na kuunga mkono jitihada za waandishi wa habari nchini kutokana na kazi wanazofanya iliyolenga kuimarisha weledi na uwajibikaji kwa viongozi wa watumishi wa umma katika sehemu zao za kazi.
Hemed alisema kuwa pamoja na kazi nzuri inayofanywa na vyombo vya habari Zanzibar lakini zipo changamoto wanazokabiliana nazo waandishi ikiwemo kukosa ushirikiano kutoka kwa baadhi ya viongozi wa serikali, taasisi za umma na Jumuiya za Kiraia kwa kuficha habari ambazo zinatoa sura mbaya ya vitendo vyao kwa maslahi yao binafsi.
“Waliowengi katika kundi hili hupenda wasifiwe tu na kupongezwa, na wengine hudiriki kuwafukuza waandishi, kuwakaripia pamoja na kuwapa vitisho pindi wanapohitaji undani wa suala lenye harufu ya uzembe, ubadhilifu wa fedha, rushwa na ufisadi,” alisema Hemed.
Aidha katika maadhimisho hayo aliwahakikishia wandishi kuwa serikali inathamini juhudi za sekta ya habari katika kuleta ufanisi na maendeleo kwa taifa.
Akizungumzia suala la kuzingatia maadili, Hemed aliwatanabahisha waandishi kufuata maaadili ya kazi zao kwa kuandika habari zenye kuzingatia ukweli kwa kufanyiwa utafiti wakitumia vyanzo mbali mbali vya kuaminika ili habari iweze kutoa matokeo sahihi kwa jamii wanayoiandikia.
“Hapa napenda kutoa wito maalum kwa waandishi wa habari kufuata maadili ya kazi zao huku wakifahamu fika dhima na dhamana yao kwa jamii na Taifa kwa ujumla,” alieleza Makamu wa Pili.
Alisistiza kuwa ni vyema kwa waandishi wakaangalia kwa umakini juu ya matokeo ya habari wanazoziandika kabla ya kuifikisha kwa jamii wanayoiandikia ili kuepusha sintofahamu kwa kuandika habari zisizokuwa na faida kwa Wananchi na taifa kwa ujumla.
Alisema ili malengo hayo yaweze kufikiwa serikali itakuwa mstari wa mbele katika kutoa ushirikiano kati yake na vyombo vya habari kwa lengo la kuijenga jamii imara yenye maelewano na mshikamano na hatimae kuifanya jamii kuwa pamoja ikiwa ni lengo jengine la waandishi kuiunganisha jamii.
Alisema kwa kuzingatia msemo wa habari kwa ajili ya umma inalenga kuifanya jamii kuzingatia umoja na mshikamano kwa manufaa ya watu wake hali itakayoshajiisha kupatikana kwa maendeleo kwa haraka.
Alieleza serikali inatambua umuhimu wa vyombo vya habari jambo lililopelekea kuingizwa katika katiba zake kupitia katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar huku ikifahamu vyombo vya habari ni muhimili unaosadia kujenga umoja miongoni mwa wananchi.
“Kumekuwepo kwa waandishi wanaokuza mambo madogo kuwa makubwa, wanatoa habari ambazo hazijafanyiwa utafiti, zipo habari za uwongo ambazo zina lenga la kupandikiza mbegu ya fitna, chuki na uhasama, huu sio uwandishi wa habari unaokubalika na ni wa hatari,” alisema Hemed
Alielezea faraja yake kwa kuona wanahabari wenyewe kupitia jumuiya zao zilizoratibu maadhimisho hayo ikiwemo Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA) ofisi ya Zanzibar, Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jumuiya ya Waandishi wa Habari za maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA), Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC) na Klabu ya Waandishi wa habari Pemba (PPC).
“Ni imani yangu sheria itakapokuwa tayari itaweka mazingira rafiki ya waandishi wa haabri kufanya kazi zao kwa weledi na umahiri na niiombe wizara iharakishe mchakato wa kuikamilisha kwa kufuata taratibu zote,” alisema Hemed.
Nae, Kaimu Waziri wa Habari, Utamuduni Sanaa na Michezo ambae pia ni Waziri wa Utaii na Mambo ya Kale, Leila Mohamed Mussa, aliwataka waandishi wa habari kutambua nafasi zao kwa kuzingatia utaalamu katika utendaji wao wa kazi ili kujitofautisha na watu wa kawaida.
Alisema kutokana na maendeleo ya teknojia, kila mtu anaweza kutoa habari kupitia njia tofauti hivyo wanahabari wanapaswa kujitofautisha kwa kutoa habari zilizofanyiwa utafiti ili kuleta manuafaa kwa umma kama ulivyo ujumbe wa maadhimisho hayo.
Aidha, Leila aliwataka waandishi wa habari wanaochipukia kujifunza zaidi kutoka kwa waandishi wa habari wakongwe kwa lengo la kupata uzoefu na kuongeza ujuzi wa kazi zao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo, Farouk Karim, alisema Lengo kuu la kudhihirisha siku hiyo ni lenga kuonyesha kuwa vyombo vya habari vilivyopo nchini vinafanya kazi kwa mashirikiano na serikali.
Mwenyekiti huyo wa Kamati alieleza kwamba waandishi wanaweza kutoa mchango mkubwa katika kukuza maendeleo ya nchi kwa kuhimiza dhana ya uwajibikaji pamoja na kufichua maovu yanayofanywa na watu wasiokuwa waaminifu.
Aidha alimshauri Makamu wa Pili wa Rais, akiwa mtendaji mkuu wa serikali kuangalia uwezekano wa kuongezazawadi kwa waandishi wa habari ikiwa ni pamoja na kutoa viwanja kama wanavyofanyiwa waandishi wa maeneo mengine ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzanaia wazo ambalo lilikubaliwa na kiongozi huyo.
Katika maadhimisho hayo, Hemed pamoja na waziri lela kwa wakati tofauti walikabidhi tuzo za uandishi wa habari wa umahiri kwa waandishi waliofanya vizuri katika maeneo tofauti na kushauri kuingizwa kwa tuzo maalum inayohusiana na masuala ya uwajibikaji.
Katika tuzo hilo, Mwanahabari Salum Vuai issa aliibuka mshindi wa kwanza katika uandishi wa habari za kodi na maendeleo na habari za uchumi wa buluu iliyopewa jina la Dk. Hussein Ali Mwinyi waliyoishikilia kwa pamoja na Rehema Juma Mema wa Hits FM, Asya Hassan Bakar wa Zanzibar leo alitwaa tuzo ya habari za seriklai ya umoja wa kitaifa iliyopewa jina la Maalim Seif Sharif Hamad.
Aidha tuzo ya maswala ya jinsia, iliyopewa jina la tuzo ya Mama Maryam Mwinyi ilichukuliwa na Wahida Nassor wa Hits FM wakati Tunzo ya uandishi wa habari za Rushwa na Uhujumu Uchumi ilichukuliwa na Mwanahabari Shah Salum Msabah kutoka Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) tuzo ambazo zinatarajiwa kuwa endelevu.