SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema mabadiliko ya tabia nchi yanayoendelea kujitokeza duniani yameanza kuathiri kilimo cha Mwani katika kina kidogo cha maji ya bahari.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Saada Mkuya Salum, wakati akijibu suali la Mwakilishi wa Jimbo la Mkwajuni, Sulubu Kidogo Amour, aliyetaka kujua kama serikali inatambua kama kuna mabomba ya maji ya kemikali yanazomwagwa baharini.

Amesema kutokana kuongezeka la joto katika kina kidogo cha maji baharini imesababisha kilimo cha Mwani kuathirika na kupungua kwa uzalishaji wa zao hilo sambamaba na kupungua na kipato cha wananchi wanaojishughulisha na kilimo hicho.

“Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2020 na Shirika la Chakula Duniani (FAO) kwa kushirikiana na Idara ya Maendeleo ya Uvuvi Zanzibar, imebaini kuwa tatizo la kufa kwa Mwani katika maji madogo linasababishwa zaidi na kuongezeka kwa joto kwenye maji hayo, na kunakosababishwa na kuongezeka kwa joto duniani ambalo linatokana na mabadiliko ya kidunia ya tabia ya nchi “alisema.

Alisema serikali kwa kulitambua tatizo hilo, Wizara ya Kilimo, Mifugo, Maliasili na Uvuvi, ilitoa vifaa mbali mbali kwa baadhi ya wakulima wa Mwani, vikiwemo vihori vya kuwasaidia wakulima waweze kwenda kwenye maji makubwa kwa ajili ya ukulima huo .

Hivyo serikali kupitia  Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi,  alisema itaendelea kuwaunga mkono wakulima wa mwani Unguja na Pemba, kwa kuwapatia vifaa vitakavyowawezesha kwenda kwenye maji makubwa kwa ajili ya ukulima wa huo.

Aidha, Ofisi ya Makamu ya Kwanza wa Rais, kwa kushirikiana na Wizara ya Biashara na Viwanda kupitia Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) alisema itaandaa viwango vya maji yanayotoka kwenye mabwawa ya kuogolea, ili kuwa na uhakika na usalama katika maendeleo ya sekta ya kilimo.

Alisema kwamba serikali itaendelea kufatilia maji yanayotoka katika mabwawa ya kuogelea ili kuhakikisha suala la utunzaji wa mazingira linazingatiwa ikiwemo kuratibu maji yaliyotumika ili kuepusha madhara kwa wakulima wa mwani.