NA MWAJUMA JUMA
SERIKALI imesema kuwa itaendeleza juhudi za kuhakikisha kuwa changamoto ya ajira inapungua au kuondoka kabisa hapa nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Abdalla Hussein Kombo katika hafla ya kukabidhi vyeti kwa wahitimu 97 wa mafunzo ya muda mfupi ya kukuza ujuzi ya awamu ya kwanza yaliyofanyika huko Amaan mjini Unguja.
Mafunzo hayo ya miezi sita ambayo yaliwashirikisha wanafunzi 100 kutoka wilaya 11 za Zanzibar walijifunza useremala, ufundi wa vifaa vya umeme vikiwemo mafriji na vipoza hewa yalisimamiwa na Wizara ya Nchi Ofisi ya Kazi, Uchumi na Uwekezaji kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO).
Alisema miongoni mwa jitihada zinazochukuliwa na Serikali mbali ya juhudi za kutanua uwekezaji, suala la kukuza ujuzi limepewa umuhimu wa pekee ili vijana waweze kujiajiri, kuwa wenye uwezo wa kuzalisha zaidi na hatimae kunyanyua pato la taifa.
Kombo alisema kwa mujibu wa utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya Kazi wa mwaka 2014 ambao ni wa mwisho kiwango cha ukosefu wa ajira kwa ujumla ilikuwa ni asilimia 14.3 ambapo kwa vijana wenye umri wa miaka 15-24 ni asilimia 27.0 na kwa vijana wenye umri wa miaka 15-34 ni asilimia 21.3.
Aidha alisema utafiti huo pia ulibainisha kuwa kiwango cha vijana wasio katika ajira hawatambuliwi na mfumo wa elimu na hawako katika mafunzo kwa vijana wa umri wa miaka 15-24 asilimia 14 na kwa umri wa miaka 15-35 asilimia 14.6.
“Napenda mfahamu kwamba nyinyi ndio vijana wa mwanzo kuhitimu katika programu hii ambao mmetoka katika wilaya 11 za Zanzibar na mmejionea wenyewe faida mliyoipata, ni wajibu wenu kuthamini juhudi za serikali ili muwe chachu ya mabadiliko katika jamii zenu hasa katika kupambana na changamoto ya ajira”, alisema.
Kombo ambae ni Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi aliwataka vijana hao watambuwe kwamba ujuzi walionao hautakuwa na thamani endapo hawatoutumia ipasavyo kwa kufanya kazi zinazoendana na ujuzi walionao na kutoa ujuzi kwa vijana wenzao waliokosa fursa hiyo.
Akisoma risala ya wanafunzi waliohitimu mafunzo hayo Zulfa Salum Mohammed alisema katika mafunzo hayo walikabiliwa na changamoto mbali mbali ambazo serikali inapaswa kuzifanyia kazi.
Alizitaja changamoto hizo kuwa ni uhaba wa vifaa vya mafunzo, muda kuwa mfupi wa mafunzo, mazingira hatarishi pahala pa kazi, kutokuwa na mfumo rafiki kwa watu wenye mahitaji maalumu na baadhi ya taasisi kutokuwa tayari kuwapokea wakati wa Mafunzo ya vitendo.
Mapema Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ajira Suleiman Ali alisema jumla ya vijana 556 wakiwemo wanawake 88 na wanaume 468 waliomba kupatiwa mafunzo hayo ambapo 449 ndio waliokuwa na vigezo wakiwemo wanawake 76 na wanaume 373.
Alisema kuwa katika mchakato wa kupatikana wanafunzi hao Idara ilihitaji vijana 368 wakiwemo wanawake 66 na wanaume 302 ambao walifanyiwa usaili na kupatikana vijana 100 ambao ndio hao waliohitimu mafunzo hayo, wakiwemo watu wenye mahitaji maalumu.