NA ALLY HASSAN, DOMECO

WIZARA ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, imesema sababu zinazopelekea serekali kutoruhusu usajili wa michezo wa ngumi (Kick Boxing,Boxing) hapa Zanzibar, ni kutokana na maelekezo yaliotolewa na Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume ya kuzuia mchezo huo.

Kaimu Waziri wa Wizara hiyo, Lela Muhamed Mussa, alisema hayo wakati akijibu suala lililoulizwa na mwakilishi wa Jimbo la Mpendae Shaban Ali Othman, alipotaka kujua ni sababu gani za msingi zinazoipa ugumu serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia wizara husika, kuruhusiwa mchezo wa ngumi (Boxing) pamoja na mchezo wa (Kick-boxing) ili kuongeza ajira pamoja na kukuza na kuutangaza utalii wetu kupitia mabondia.

Kaimu Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo Lela Mohamed Mussa, alisema serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaenzi mawazo, fikra na busara za marehemu Sheikh Abeid Amani Karume, ambazo zilizuia mchezo huo  kufanyika katika visiwa vya Zanzibar.

Alisema wizara bado inaendelea na utaratibu wa kisheria wa kuhakikisha unafanya marekebisho ya sheria, ambazo zinaleta vikwazo ikiwemo mchezo wa ‘Kick Boxing’, pamoja na hayo wizara itahakikisha inaangalia maslahi ya mchezo huo na ya nchi kwa ujumla na ndipo itafanya maamuzi ya kuruhusu mchezo huo.

Kaimu huyo alieleza mchezo huo unaweza kuruhusiwa pale ambapo serikali itafuta kauli za muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar kwa mujibu wa taratibu za kisheria zitakazoonekana zinafaa.

Akijibu suala la nyongeza la mwakilishi wa Jimbo la Mpendae, Shaaban Ali Othman, alipotaka kujua ni lini serikali itatengua kauli ya Rais wa kwanza kwa manufaa ya nchi.

Alisema serekali ikiona suala hilo linafaa basi itatengua kauli hiyo ya muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar.

Akijibu suala la nyongeza lililoulizwa na mwakilishi wa Jimbo la Chwaka, Issa Haji Ussi Gavu, aliyehoji kuna kikwazo gani kinacho ikwaza Zanzibar kushiriki ‘Kick Boxing’.

Alisema sababu ni kauli iliyotolewa na Rais wa Kwanza wa Zanzibar na serikali itaangalia jinsi gani mchezo huo utaruhusiwa kuchezwa Zanzibar.