KHAMISUU ABDALLA NA MARYAM HASSAN

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa mwaka wa Fedha 2021/2022, imelenga kufanya mageuzi makubwa katika sekta  hiyo.

Kauli hiyo ilitolewa na waziri wa Wizara hiyo Simai Mohammed Said, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2021 katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi uliopo Chukwani.

Alisema mageuzi hayo ni pamoja na kuzipatia skuli zote za maandalizi, msingi na sekondari ruzuku za uendeshaji na kuwapatia wanafunzi vifaa ikiwemo vikalio, mabuku, vifaa vya kusomeshea na kufundishia.

Aidha alisema mageuzi mengine ni kuimarisha miundombinu na mazingira ya kujifundishia na kujifunzia kwa kujenga madarasa 485 yakiwemo madarasa 300 yaliyoanzishwa na wananchi na madarasa 185 mapya.

Waziri huyo alieleza kuwa mbali na hayo serikali itajenga skuli tano za maandalizi katika kila mkoa, skuli tatu katika maeneo ya Kijichi, Nanguji na Pujini.

Alisema ujenzi huo pia utahusisha skuli tisa za sekondari katika maeneo ya Mtopepo, Mfenesini, Gamba, Bumbwini, Chukwani, Donge, Kifundi, Mfikiwa na Mwambe na skuli mbili maalum za mjumuisho katika Mkoa wa Mjini Mgharibi na mkoa wa Kusini Pemba.

Simai alisema pia katika bajeti hiyo watajenga skuli moja ya ufundi Nungwi wilaya ya Kaskazini ‘A’, na ujenzi wa maabara katika skuli 11 za sekondari ikiwemo Fukuchani, Jongowe, Chukwani, Bumbwini, Machui, Jendele, Shumba, Uwondwe, Chanjamjawiri, Chambani na Wambaa.

Hata hivyo alisema pia watafanya ukarabati mkubwa wa skuli za sekondari, ikiwemo Paje, Mtule, Uzini, Haile salassie, Chwaka Tumbe, Dk. Omari Ali Juma na Chuo cha Kiislam Kiuyu.

Alisema wizara pia inatarajia kuimarisha huduma za maktaba kuu ya kisasa katika wilaya ya Kaskazini ‘A’, na ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Amali katika mkoa wa Mjini wa Magharibi na vituo vitano vya Mafunzo ya Amali vya Wilaya ya Kaskazini ‘B’,Magharibi ‘A’ Kati , Mkoani na Micheweni .

Mageuzi mengine alisema ni ujenzi wa dahalia mbili katika skuli ya Chwaka Tumbe, na Paje Mtule, aidha watatekeleza program ya lishe kwa skuli zote za maandalizi, za serikali na skuli 36 za msingi , kuimarisha mazingira rafiki ya skuli kwa watoto wote wakiwemo wenye mahitaji maalum.

Waziri Simai aliliomba baraza hilo kumuidhinishia jumla ya shilingi bilioni 265,549,743,000 kwa mwaka  wa fedha 2021/2022, ili kuiwezesha wizara yake kutekeleza majukumu yaliyopangwa.

Baada ya wajumbe wa Baraza hilo kuijadili bajeti hiyo na waziri huyo kufanya majumuisho waliidhinisha bajeti hiyo.