NA TIMA SALEHE, DAR ES SALAM

Mabingwa wa ligi kuu Tanzania bara Simba S.C leo inatarajiwa kushuka dimbani kuwakabili Keizer Chiefs katika mchezo wa mkondo wa pili wa robo fainali ya ligi ya mabingwa Afrika.

Mchezo huo utakaopigwa katika uwanja wa benjamin mkapa, Simba itakuwa na kibarua kigumu cha kubadilisha matokeo ili kusonga mbela baada ya kukubali kipigo cha magoli 4 – 0 katika mchezo wa awali uliochezwa Uwanja wa FNB, nchini afrika kusini.

Kocha Mkuu wa Kaizer Chiefs, Gavin Hunt,aliewasili nchini juzi na klabu yake, atakuwa na kibarua cha kulinda ushindi wao huku  Kocha Mkuu, Didier Gomes wa Simba akiwa na kazi ya ‘kupindua meza’ jambo linaloufanya mchezo huo kuwa mgumu kwa timu zote mbili.

Akizungumza mara baada ya kuwasili, Mkurugenzi wa Masoko wa Kaizer Chief, Jessica Motaung, alieleza pamoja na kujiandaa vyema na mchezo huo, hofu yao ya kwanza ni suala la Corona ambapo, amesema kuwa wana wasiwasi juu ya vipimo vya Corona huku akibainisha kwamba wao wapo vizuri.

“Sina wasiwasi juu ya mapokezi ambayo tumeyapata Dar es salam. Uzuri ni kwamba tayari wachezaji wetu wote wapo vizuri kwa mchezo na hawana virusi vya Corona,” alisema Jessica.

Aidha wachezaji wa klabu hiyo, walisema wanaamini kuwa mchezo huo utakuwa mgumu ila wana wasiwasi na waamuzi wa mchezo huo pamoja na hali ya hewa kuwa tofauti kidogo na ya nchini kwao.

Akizungumza na vyombo vya habari, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, aliwatoa hofu washabiki wa timu hiyo na kuahidi kuwa klabu hiyo itaibuka na ushindi.

Alisema dhamira ya klabu hiyo ni kusonga mbele katika hatua ya nusu fainali na kwamba wana uwezo wa kuibuka na ushindi wa mabao 5 – 0 ikiwa wachezaji wataamua hilo.