NA MWANDISHI WETU
BAADA ya Simba kushindwa kufuzu nusu fainali ya ligi ya mabingwa Afrika licha ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Kaizer Chiefs, kocha mkuu Didier Gomes amesema wamepata somo na msimu ujao watakuwa bora zaidi.
Gomes alisema kupoteza kwa idadi ya mabao 4-0 katika mchezo wa mzunguko kwanza umewapa kazi kubwa ya kupindua matokeo ambayo si rahisi hasa kwenye hatua hii.
Mfaransa huyo aliongeza kuwa katika mchezo wa kwanza uliopigwa Afrika Kusini wiki iliyopita, hawakuwa wazuri kwenye kuzuia na kusababisha kuruhusu idadi kubwa ya mabao, kitu ambacho kimewapa somo na msimu ujao kutushiriki haitajirudia.
“Tulikuwa na malengo ya kutinga nusu fainali lakini imeshindikana. Tumejifunza na tukipata nafasi ya kushiriki msimu ujao tutakuwa bora zaidi,” alisema Gomes.
Gomes amewasifu wachezaji kwa kupambana muda wote na kujitoa kwa ajili ya timu, katika mchezo wa juzi kitu ambacho kinamfanya kujivunia kufanya nao kazi.
“Wachezaji walipambana kwa ajili ya timu, walifanya kila kitu kwa ajili ya timu lakini bahati haikuwa upande wetu kwa kweli najivunia kufanya nao kazi,” alisema Gomes.