NA MARYAM HASSAN

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inathamini michango ya vyama vya ushirika katika kuimarisha hali za maisha ya wananchi kiuchumi na kijamii.

Kauli imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga, wakati akifungua mkutano wa wadau wa mkakati wa kuimarisha vyama vya ushirika Zanzibar katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul wakil Kikwajuni mjini Zanzibar.

Alisema takwimu zinaonesha kwamba zaidi ya watu 5,000 wameajiriwa kupitia vyama hivyo katika sekta za usafirishaji, ubebaji wa mizigo, upakuaji na uteremshaji wa mizigo katika maeneo ya baharini na viwanja vya ndege.

Soraga alisema kupitia SACCOS mbali mbali zaidi ya wanachama 28,000 wamepata mikopo na wanaendesha shughuli mbali mbali za kibiashara na kupitia vyama vya uzalishaji 2,622 vimetoa ajira binafsi kwa wananchi zaidi ya 13,110.

“Hivi sasa vyama vya ushirika vinawaunganisha wananchi na vinatoa huduma nyingi ikiwemo ya mikopo, mafunzo, ushauri na kujipatia riziki zao za halali jambo ambalo ni la faraja sana,” alisema Soraga.

Sambamba na hayo alisema imefika wakati sasa kwa vyama vya ushirika kuchangia upatikanaji wa ajira 300,000 zilizoahidiwa na serikali na kwamba ina matarajio ya kuona vyama hivyo vinakuwa imara na kuwahudumia wanachama wake kwa ufanisi.

“Tunatarajia kupunguza manung’uniko kwa wananchi kwa kuhakikisha kuwa wanatendewa haki na si kunufaika kwa watu wachache,” alisema.

Aidha alisema wanatambua kuwa vyama vingi vimekuwa viikikumbwa na migogoro mbali mbali ambayo inatokana na utendaji mbovu, hivyo aliwaomba viongozi hao kuondoa migogoro hiyo ambayo haileti tija.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya vyama vya ushirika, Khamis Daudi Simba, alisema kuwepo kwa vyama vya ushirika katika shehia au majimboni kumewawezesha wananchi kujiendeleza kimaisha na kiuchumi.

Alieleza kuwa azma ya serikali ni kuviendeleza vyama hivyo ili kuongeza tija na kuimarisha mapato ya serikali.

Kwa upande wake Afisa Sheria wa Idara ya Msaada wa kisheria, Amina Mzee Haji, akitoa neno la shukurani alisema watayatekeleza maagizo waliyopewa ili kuleta mabadiliko ya kihistoria katika vyama vyao kwa lengo la kuleta maendeleo.