NA NASRA MANZI, WHVUM

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Vijana ,Utamaduni na Michezo Khamis Abdalla Said, amesema serikali itajenga miundo mbinu ya michezo, ili watu wenye ulemavu kushiriki katika mashindano mbali mbali ndani na nje ya nchi.

Akifungua mafunzo ya makocha wa Michezo Jumuishi yaliyoandaliwa na kamati ya ‘Special Olympics Tanzania’ (SOT) kwa kushirikiana na ‘Special Olimpics Zanzibar ‘(SOZ) ,yaliyofanyika katika ukumbi wa kitengo cha watoto wenye ulemavu wa akili  huko skuli ya msingi Jang’ombe.

Alisema lengo la serikali kutoa fursa kwa watu wenye ulemavu pamoja na wananchi katika kushiriki huduma za kiuchumi na kijamii, ikiwemo michezo lakini pia kutambua umuhimu wa watu hao  na mahitaji yao kama watu wengine.

Hata hivyo alisema serikali inaazimia kusaidia vyama vya michezo vya Zanzibar kupata uwanachama wa kitaifa katika mashirika mbali mbali duniani, ili fursa zinazotolewa ziwanufaishe wachezaji wa Zanzibar .

Aidha amewataka makocha kuwa na program maalum zisizo za ubabaishaji za kuwaandaa na kuwatayarisha wanamichezo wenye ulemavu,  kuwa na sifa na uwezo wa kushiriki katika mashindano ya ndani na nje ya nchi.

” Dira ya maendeleo ya Zanzibar pia inataka kuona ifikapo mwaka 2030 miaka 10 kutoka sasa Zanzibar inapata medali za kimataifa 100 kwani ‘special olympics’ Zanzibar ina jukumu la kuandaa wanamichezo kuleta medali hizi” alisema

Makamu Mwenyekiti wa ‘Olympics’ Zanzibar Omar Iddi wakati akisoma risala alisema Chama cha Michezo kwa ajili ya Watu wenye Ulemavu wa Akili Zanzibar kimepeleka jumla ya wanamichezo wanane nje ya nchi.

Alizitaja nchi hizo ni Marekani, Ireland, Ugiriki, Sweeden, Misri, Bahrain na Afrika Kusini, ambako waliwakilisha vyema na kurudi na medali za fedha,dhahabu na hivyo kuitangaza Zanzibar na Tanzania.

Alisema kwa sasa wanajiandaa kupeleka wachezaji 38 pamoja na makocha  mkoani Mwanza Tanzania Septemba mwaka huu kwa ajili ya kushiriki mashindano ya Taifa.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa ‘Special  Olympics’ Tanzania Charles Rays alisema ni vyema watu wenye ulemavu kushiriki katika mashindano na wanamichezo ambao hawana ulemavu ili kusudi kujiona sawa na wenzao kwa ajili ya kuimarisha na kuibua vipaji vyao.

Mafunzo hayo ya siku mbili ambayo jumla ya makocha   30 wakiwemo wanaume na wanawake wameshirikishwa kwa lengo la kuwawezesha wanamichezo wenye ulemavu.