NA LAYLAT KHALFAN

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masuod Ali Mohammed, amekabidhi majukumu ya taasisi zilizokuwa zimegatuliwa kwa wizara.

Hatua hiyo inafuatia taassisi hizo kurudishwa katika wizara zao za asili hivi karibuni baada ya kugatuliwa na kupelekwa katika mamlaka za serikali za mitaa baada ya serikali kufanya tathmini juu ya mwenendo mzima wa ugatuzi.

Wizara zilizozikabidhiwa majukumu, mali na rasilimali watu ni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee, Wanawake na Watoto, Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji maji, Maliasili na Mifugo na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Masoud alisema imani yake ya kubadilisha mfumo huo wa ugatuzi ni kupata ufanisi mkubwa kwa jamii iliyowazunguka sambamba na kuwapunguzia changamoto katika mahitaji yao.

“Mfumo huu umekabiliwa na changamoto nyingi kiasi ambacho tunalazimika kurudisha majukumu katika sekta mama kwa lengo la kwenda kutekeleza huko,” alisema.

Waziri Masoud, alisema miradi yote ambayo haijakamilika wataikabidhisha pamoja na watumishi ambapo hali hiyo itaanza rasmi katika mwaka wa fedha ujao.

Akizungumza katika makabidhiano hayo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Simai Mohammed Said, alisema watapanga mikakati kuhakikisha wanawalea watoto katika misingi bora ya kielemu ili kufikia azma ya kuinua ubora wa elimu.

Alisema hali hiyo itafikiwa iwapo watakua wanafanyakazi kwa mshirikiano kwa kuwasimamia wanafunzi ili kinachosomeshwa kiwe na uhakika badala ya kusomesha kimazoea.