NA VICTORIA GODFREY

TIMU ya Tambaza Youth imeibuka na ushindi wa mabao 2 -0 dhidi ya Tanzebra  katika mchezo wa Jiandae Cup uliofanyika juzi kwenye Uwanja wa Airwing, Dar es Salaam.

Wafungaji wa mabao ya Tambaza Aboubakari Joka aliipatia ushindi wa bao la kwanza dakika ya 59  akifuatiwa na Devis Emmanuel  aliyefunga bao la pili dakika ya 75 .

Akizungumza na gazeti hili Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Wilaya ya Ilala(IDFA) Daud Kanuti, alisema mashindano yanaendelea kwa kasi kwa timu shiriki kuonyesha umwamba.

Alisema mashindano  yanayoendelea timu zinaimarika na kuonyesha viwango vya ushindani kutokana na kila mmoja anataka apate ushindi katika michezo yake.

” Tukiwa tunaelekea katika ligi zetu, tunaamini zitafanyika kwa ushindani mkubwa baada ya kumaliza mashindano hayo,ndio maana tumetoa fursa kwa wachezaji kujiandaa kwa kucheza michezo kama hii, ambayo itakuwa kipimo cha kubaini mapungufu na makocha kwenda kuyatafutia tiba,” alisema Kanuti.