Aliifungia Simba magoli matatu ikishinda 5-0 nchini Zambia
NA MWANDISHI WETU
JE unamkumbuka Thuwein Ally Waziri. Ni mshambuliaji wa zamani wa klabu ya soka ya Simba ya Dar es Salaam na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Mshambuliaji huyo aliyekuwa maarufu kwa wanasoka wenzake kwa jina la utani kama ‘Guu la Kushoto’, kutokana na kutumia kwake mguu huo enzi zake, kwa sasa amestaafu soka na anaishi nchini Oman.

Thuwein ni kati ya wachezaji bora waliowahi kutokea Tanzania, ambaye alikuwa akikonga nyoyo za mashabiki kwa jinsi alivyokuwa akiburuza kandanda kwa guu lake la kushoto.
Ni guu lake hilo la kushoto lililokuwa likiwapiga chenga za maudhi mabeki mahiri na kuwatungua mabao matamu makipa hodari, enzi zake akicheza soka nchini.
Mashabiki wanaposema siku hizi hakuna wachezaji Tanzania, wanakuwa wana hoja, kwa sababu wanakumbuka vyema wakali kama Thuwein waliifanyia nini nchi yao enzi zao.

MFUNGAJI BORA WA STARS NIGERIA 1980

Sahau kuhusu Peter Tino aliyefungia Stars bao muhimu katika mechi dhidi ya Zambia mjini Ndola, mwaka 1979 na kufanya sare ya 1-1, hivyo kuipa Tanzania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Nigeria mwaka 1980.
Pia sahau kuhusu Mohamed Adolph Rishard aliyefungia Stars bao pekee katika mchezo wa kwanza dhidi ya Zambia mjini Dar es Salaam, hivyo kwa matokeo ya 1-1 kwenye mechi ya marudiano mjini Lusaka, Tanzania ikajikatia tiketi ya kwenda Nigeria mwaka 1980.

Lakini, pia sahau kuhusu Juma Mkambi aliyefunga bao la kufutia machozi wakati Stars inachapwa 3-1 Machi 8, mwaka 1980 na wenyeji Nigeria kwenye mechi ya ufunguzi wa fainali za Nigeria iliyokuwa ya kundi ‘A’ kwenye fainali hizo za Kombe la Mataifa ya Afrika.
Mshambuliaji, Thuwein Ally, aliifungia Stars mabao yote matatu kwenye fainali za Nigeria, moja la kufutia machozi kwenye mechi dhidi ya wenyeji, Nigeria, jengine dhidi ya Misri na la kusawazisha katika mchezo dhidi ya Ivory Coast.

Tanzania ilipangwa kwenye kundi la kifo ‘A’ lililokuwa likitumia Uwanja wa Surulele mjini Lagos dhidi ya wenyeji, Nigeria, Misri zilizofuzu kuingia raundi ya pili na Ivory Coast ambayo kama Stars ilifungashiwa virago baada ya mechi za kundi hilo.
Machi 8, mwaka 1980 kwenye Uwanja wa Surulele, Thuwein alifunga bao lake dakika ya 54 na kufanya Nigeria iwe mbele kwa 2-1 baada ya kuongoza kwa 2-0 tangu dakika ya 35, Oyendika alipofunga bao la pili kufuatia Lawal kufunga la kwanza dakika ya 11, lakini Odegbami alishindilia msumari wa moto kwenye jeneza la Stars dakika ya 85.

Machi 12, mwaka 1980, Thuwein Ally, aliifungia Stars bao katika dakika ya 86, likiwa ni la kusawazisha baada ya Hassan Shehata, ambaye aliwahi kuinoa Misri, kuwafungia Mafarao hao bao dakika ya 32 na Mosaad Nour dakika ya 38.
Thuwein tena Machi 15, 1980 katika mchezo wa mwisho wa kundi hilo la Stars, aliifungia timu hiyo bao dakika ya 59, kufuatia Kobenan kuifungia Ivory bao la mapema dakika ya saba.

Kwa mabao hayo, jina la Thuwein Ally, likawa miongoni mwa majina makubwa na ambayo hayatasahaulika katika soka ya Tanzania.
Akizungumzia mashindano hayo ya Nigeria, Thuwein, alisema, Stars ilikwenda huko bila ya maandalizi ya kutosha, licha ya ziara ya mafunzo nchini Mexico.
“Kule timu zilikuwa zimeandaliwa zaidi kuliko sisi, japokuwa tulikwenda Mexico kwa maandalizi kabla ya mashindano kuanza, lakini tulionekana kama bado kiwango chetu kiko chini.

Kwani tulitumia muda mwingi kuwasoma wenzetu kabla ya kuanza kucheza soka, na zaidi tulikuwa tukiibuka na kucheza vizuri kipindi cha pili na hata magazeti ya Nigeria yalikuwa yanaandika hivyo,” anasema.
Ingawa alikwenda Nigeria na Stars kama mshambuliaji wa Simba, lakini, kisoka Thuwein aliibukia visiwani Zanzibar, alikozaliwa na kukulia.

‘HAT-TRICK’ YA MUFULIRA 1979

Kwani nini mashabiki wa Simba hawatamsahau Thuwein Ally. Kikubwa ni vitu vyake alivyofanya nchini Zambia mwaka 1979, Simba ilipokuwa ikirudiana na Mufulira Wanderers katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, sasa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba ilikwenda Zambia ikiwa mashabiki wake wamekwishakata tamaa ya kusonga mbele, baada ya kipigo cha nyumbani cha mabao 4-0 ilichokipata kutoka kwa Wazambia hao mjini Dar es Salaam.

Lakini, katika hali iliyowastaajabisha wengi, kwenye mchezo wa marudiano Wekundu wa Msimbazi, waliibuka na ushindi wa mabao 5-0 mjini Lusaka, matatu yakifungwa na Thuwein Ally Waziri na George ‘Best’ Kulagwa.
“Kwa kweli mchezo ule kuna vitu viwili au vitatu vilitufanya tushinde, kikubwa ni kwamba wachezaji wenyewe tulisema kwamba, kama hawa wametufunga 4-0 nyumbani, na sisi tutakwenda kuwafunga kwao zaidi ya walivyotufunga.

Na kweli, tulipofika kule pamoja na kuzomewa na Wazambia, walikuwa wakitutambia sisi tumekwenda kufungwa mabao mengine sita na kila aina ya kejeli, lakini sisi tulikuwa na dhamira moja tu, kucheza kwa bidii ili tushinde.
Tulipeana majukumu, kila mtu acheze kwa juhudi, mabeki wasiruhusu magoli na kule mbele tutafute mabao kwa jitihada kubwa na tukafanikiwa, nakumbuka mimi peke yangu nilifunga magoli matatu safi, mengine alifunga George Kulagwa kama sikosei (mawili),”anakumbuka Thuwein.

Kwa matokeo hayo, Simba ilifuzu kuingia raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kukutana na Racca Rovers ya Nigeria.
Mchezo wa kwanza uliofanyika Dar es Salaam na timu hizo zilitoka sare ya bila ya kufungana 0-0 na ziliporudiana mjini Lagos, Rovers walishinda 2-0, hivyo Simba kutolewa.
Mshambuliaji huyo nyota wa zamani wa Tanzania, alizaliwa Aprili 6, mwaka 1959 visiwani Zanzibar na alipata elimu yake ya Msingi katika Skuli ya Darajani, kabla ya kujiunga na Sekondari ya Haille Selassie.

Mbali na kucheza soka skuli, Thuwein pia alichezea timu za watoto za Everton na Small Simba kabla ya kusajiliwa na mabingwa wa zamani wa Tanzania, Malindi iliyokuwa Ligi Daraja la Kwanza Zanzibar, sasa Ligi Kuu mwaka 1975.
Aliichezea Malindi hadi mwaka 1979 alipohamia kwenye klabu ya Wekundu wa Msimbazi, Simba SC, ambako alicheza hadi mwaka 1982 na kutimkia Kenya kujiunga na klabu ya Belham, iliyokuwa daraja la pili kwa muda wa miezi mitatu.
Kutoka hapo, Thuwein alikwenda moja kwa moja Abu Dhabi, Falme za Kiarabu kuchezea timu ya jeshi la nchi hiyo hadi mwaka 1987 alipohamia Al Suwaiq ya Oman, ambayo aliichezea hadi mwaka 2002, alipoamua kutundika daluga zake.
Alipofika Abu Dhabi, anasema, kwamba alipata mafunzo ya kijeshi na kuajiriwa na jeshi la Abu Dhabi, alilolitumikia hadi mwaka 1992 na kustaafu.