NA ABOUD MAHMOUD

SHERIA ni jambo muhimu sana katika nchi yoyote ile dunia kwa kuwa huweka mfumo wa utawala ikiwa ni pamoja na kila kitu kusimamiwa au kufanywa kwa misingi ya kisheria kutegemea na nchi husika.

Kwa hakika hakuna mtu alie juu ya sheria na ndio maana tunawaona viongozi mbalimbali wakichukuliwa hatua za kisheria kwa yale mambo wanayoyafanya kinyume na sheria.

Umuhimu wa sheria huonekana pale linapotokea tatizo linalotaka ufumbuzi jambo ambalo wakati mwengine ni lazima sheria ichukuwe mkondo wake.

Takriban duniani kote kwa kila nchi kuna sheria zao zilizotungwa au zinazoendelea kutungwa kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wake wanafahamu umuhimu wa jambo hilo.

Kuna vyombo mbalimbali vya kutunga sheria hutegemea utaratibu wan chi husika kwa mfano hapa Tanzania bunge na baraza la wawakilishi ndilo linalohusika kutunga sheria, hata hivyo, ziko sheria ndogondogo zinazotungwa na mabaraza ya manispaa nakadhalika.

Kwa mfano hapa Zanzibar watu wengi hawajui hata kwa ufupi kuhusiana na sheria jambo ambalo huwakoseha haki zao nyingi.

Hivyo, kwa makusudi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya awamu ya saba chini ya uongozi wa Dk Ali Mohammed Shein ilianzisha rasmi ofisi ya msaada wa kisheria ili wananchi wasiona uwelewa wa sheria kuitumia ofisi yao hasa kwa mambo yanayohitaaji msaada wa kisheria.

Kuanzishwa kwa ofisi hiyo kulikua na maana ya kuwasaidia wananchi kufahamu maswala mbali mbali ya kisheria ili kutatua matatizo waliyokuwa nayo.

Mara baada ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo ambayo ipo chini ya Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora imeweza kufanya kazi kwa kupita katika maeneo mbali mbali ya visiwa hivi ili kutoa elimu hiyo.

Takriban mikoa yote mitano ya Zanzibar ofisi ya msaada wa kisheria iliwafikia wananchi wake na kuwapata watoa msaada wa kisheria ili wananchi waweze kuhakikisha yale waliyokua wakifanyiwa hawanyiwi tena kwa mujibu wa sheria.

Ni uwazi usiopingika kuwa Ofisi ya Msaada wa Kisheria na watoa msaada wa kisheria wamefanikiwa na kufikia sehemu kubwa ambayo inastahiki pongezi kwa wanayoyafanya.

Hivi sasa kama utatembelea vijiji mbali mbali mbali vilivyokuwemo ndani ya  visiwa vyetu utaweza kukutana na wananchi ambao wamefanikiwa kupata msaada wa kisheria na kutetea haki zao.

Hii imeonesha dhahiri kwamba ofisi hiyo inafanya kazi inavyotakiwa na wananchi wameweza kufahamu nini wanachotakiwa kufanya katika kutatua matatizo yao kupitia sheria.

Ni jambo la kupongezwa kuona ofisi hiyo inayotoa msaada wa kisheria kupiga hatua kubwa kwa kuwafikia wananchi wa maeneo mbali mbali ya Zanzibar hasa kwa wakaazi wa vijijini na wanawake .

Kutokana na jitihada zinazochukuliwa na ofisi ya msaada wa kisheria Zanzibar pamoja na watoa msaada wa kisheria ni vyema wananchi kuwaunga mkono katika kufikia malengo yaliokusudiwa.

Naamini kuiunga mkono Ofisi ya msaada wa kisheria ni hatua muhimu sana kwani hii haitoisaidia ofisi hiyo peke yake bali ni kujisaidia mwenyewe mwananchi katika kujua sheria, kudai haki pamoja na kutatua matatizo yanayomkabili mtu.

Hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuitumia ofisi ya msaada wa kisheria kwa hali na mali kwa ajili ya kujifunza mambo mbali mbali yanayohusu sheria lakini pia kujiamini wakati ukiwa na kesi.

Kwa wananchi wa Zanzibar tumeona faida ya kuwepo kwa sheria kwani wengi imeweza kutusaidia katika kupambana kwenye kutatua matatizo na kudai haki ambazo zinatulazimu kuzipata kwa mujibu wa sheria.

Lakini katika visiwa hivi wapo wananchi wengi hawafahamu nini sheria au umuhimu wa sheria kutokana na mambo mbali mbali ikiwemo kukosa elimu, woga, khofu au muhali waliokuwa nao.