NA MWANDIDHI WETU, DODOMA

MWENYEKITI wa Bodi ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Profesa, Henry Fatael Mahoo, ameitaka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kujikita zaidi katika kutoa elimu kuhusu kilimo shadidi cha mpunga alichoeleza kuwa kinaweza kuongeza Tija katika sekta hiyo.

Profesa Mahoo, ameyasea hayo Jijini Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na Manenijementi na watumishi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.

Alisema kilimo hicho kinaweza kuleta Tija kwa kuongeza uzalishaji wa Tani saba mpaka 10 kwa hekta katika miradi ya kilimo cha umwagiliaji yenye uhakika wa maji. “Tutakuwa tunatekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020 – 2025 ya kufikia malengo ya ongezeko la chakula.” Alisisitiza Profesa.

Sambamba na hilo, Mwenyekiti huyo wa Bodi aliitaka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kuwajengea uwezo wataalam wake wa ndani pamoja na wakulima, ili kuweza kwenda sambamba na matumizi sahihi ya teknolojia ya kisasa katika sekta ya kilimo cha Umwagiliji.

Kwa Upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Daudi Kaali amesema kuwa, Tume inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya Kilimo cha umwagiliaji nchini ambapo kwa sasa imejikita katika kuboresha na kujenga miradi ya ujenzi shirikishi ambayo haijakamilika.

Aidha aliongeza kwa kusema kuwa,  uzalishaji wa zao la mpunga umeongezeka kwenye maeneo ya kilimo cha umwagiliaji kutoka tani laki saba na kumi na nne elfu (714,000) toka mwaka 1989/1990/2000 hadi kufikia tani milioni mbili na elfu tisa na mia mbili sabini na nne (2,009,274) mwaka 2018/2019.