HIVI karibuni Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilibadilisha matumizi ya maeneo ya mashamba ya mipira ya Unguja na Pemba kuwa maeneo ya uwekezaji wa viwanda.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kutembelea mashamba ya Selem mkoa wa Mjini Magharibi na Kichwele mkoa wa Kaskazini Unguja.

Katika ziara hiyo, taarifa zilizotolewa na wizara ya kilimo, zilionesha kwamba pamoja na kuwepo kwa mashamba hayo yenye ukubwa wa hekta 1,270, uzalishaji wa zao hilo umeshuka toka mwaka 2014 kabla ya kusita kabisa mnamo mwaka 2015.

Hali hiyo ilitokana na kutokuwepo kwa mwenendo mzuri wa mwekezaji aliyepewa mashamba hayo kwa lengo la kuyaendeleza na kusababisha uzalishaji kushuka hadi kufikia tani milioni 400 (2015) kutoka tani 4,229 za mwaka 2014.

Chambilecho maneno ya Dk. Mwinyi, ‘Kama una eneo la hekta 1,270 ambazo hazizalishi na hakuna anaefaidika’; basi uamuzi wa  kubadilisha matumizi ya maeneo hayo ni wa busara na unahitajika kuungwa mkono na kila mmoja miongoni mwetu.

Hii inatokana na ukweli kwamba katika kipindi chote ambacho mashamba hayo yamesita kuzalisha, yalibakia kama vichaka visivyo na faida kubwa kwa walio wengi na pengine kutumika kama maficho ya wahalifu.

Tunapongeza uamuzi huu hasa tukiegemea ukweli aliouanisha Rais Mwinyi kwamba wapo wawekezaji wanaohitaji maeneo kuanzisha miradi (viwanda) ambayo itawanufaisha walio wengi.

Aidha kwa kuzingatia ukweli kwamba wananchi wa Zanzibar wana matumaini makubwa na ahadi zilizotolewa na serikali ya awamu ya nane kabla na baada ya kuingia madarakani, uamuzi huu utaongeza kasi ya maendeleo ya wananchi sio wa maeneo yalipo mashamba hayo pekee bali pia nchi nzima.

Ni dhahiri miradi na viwanda hivyo vitakapoanzishwa, wananchi wengi watapata ajira na fursa ya kutoa huduma, serikali itapata kodi kutokana na uzalishaji wa viwanda hivyo na uchumi utaimarika jambo litakalotanua wigo wa utoaji huduma kwa jamii.

Tunachoamini, wakati uamuzi wa kubadilisha matumizi ya maeneo haya umeshafanyika,watendaji wa idara na taasisi zinazohusika watachukua hatua za haraka kutekeleza maagizo na maelekezo ya Dk. Mwinyi kwani hakuna muda wa kupoteza.

Hii inatokana na ukweli kwamba, muda unakwenda kasi lakini pia mambo ni mengi hasa inapozingatiwa kwamba serikali hii imeelekeza nguvu zake katika maswala ya uwekezaji kama moja ya njia za kuzalisha ajira 300,000 ilizoziahidi wakati ikiomba ridhaa ya kuingoza Zanzibar.