HARARE, ZIMBABWE

MAHAKAMA Kuu nchini Zimbabwe, imetangaza kuwa, uamuzi wa Rais Emmerson Mnangagwa kumuongezea muda Jaji Mkuu wa nchi hiyo ni kinyume cha sheria.

Wiki iliyopita, Mnangagwa alitangaza habari ya kumuongezea muda Luke Malaba wa kuwa jaji mkuu wa Zimbabwe kwa muda wa miaka mitano zaidi.

Hatua hiyo ilikuja masaa machache kabla ya Jaji Mkuu huyo kumaliza muda wake wa kushikilia cheo hicho kwa mujibu wa sheria.

Majaji wa Mahakama Kuu walisema kuwa, Malaba aliacha kuwa Jaji Mkuu wa Zimbabwe kuanzia tarehe 15 Mei, 2021 na kwamba hatua ya Rais Mnangagwa ya kumuongezea muda Malaba ni kinyume cha katiba.

Malaba analaumiwa kwa kuipendelea serikali ya Mnangagwa. Alidharau kusikiliza kesi ya kiongozi wa upinzani Nelson Chamisa ya kulalamikia uchakachuaji wa kura za urais katika uchaguzi wa mwaka 2018.

Baada ya Mahakama Kuu ya Zimbabwe kubatilisha uamuzi huo wa Rais mnangagwa, wizara ya sheria na masuala ya bunge ya nchi hiyo imetoa taarifa na kusema itakata rufaa ikilalamika kwamba Mahakama Kuu ya Zimbabwe imetekwa na nguvu za wageni na maadui wa taifa la Zimbabwe.

Kabla ya kutangaza kurefusha muda wa Jaji Mkuu, Mnangagwa alitia saini sheria ya mabadiliko ya katiba yanayompa nguvu zaidi Rais wa Zimbabwe katika uteuzi wa majaji. Hatua hiyo ya bunge la Zimbabwe ililalamikiwa vikali, lakini Mnangagwa alitia saini muswada huo na kuufanya kuwa sheria.