NA LAYLAT KHALFAN
TUME ya Uchaguzi Zanzibar, imesema uchaguzi mdogo wa Wadi ya Chwaka utafanyika Agosti 14, mwaka huu kufuatia kifo cha aliyekuwa Diwani wa Wadi hiyo, Mlenge Khatib Mlenge.
Akitoa taarifa hiyo Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mabruk Jabu Makame katika mkutano wa wadau wa uchaguzi uliofanyika ukumbi wa Chuo cha Fedha Chwaka Wilaya ya Kati Mkoa wa kusini Unguja.
Alisema kutokana na tukio hilo, tume itafanya uteuzi wa wagombea kwa ajili ya uchaguzi mwengine ifikapo Julai 28, mwaka huu.
Aidha, Mabruk alisema wagombea walioteuliwa na vyama vyao wataanza kuchukua na kurejesha fomu za Uteuzi Julai 21 mpaka Julai 27, 2021 ambapo kampeni zitaanza Julai 29 hadi Agosti 12 mwaka huu.
Katika taarifa yake hiyo Makamu alisisitiza kuwa uchaguzi huo kwa mujibu wa sheria hautakuwa na upigaji wa kura ya mapema na kuwataka wananchi, vyama vya Siasa, wapiga kura na wadau wengine wa uchaguzi kushiriki kuendelea kudumisha amani wakati wa matayarisho hadi kukamilika kwa uchaguzi huo.
Kwa upande wake Mkuu wa Kurugenzi ya Rasilimali watu, Mipango na Uendeshaji Saadun Ahmed Khamis, alisema tume imemteua Said Ramadhan Mgeni kuwa Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Chwaka akisaidiwa na Jaffar Juma Jihadi.
Saadun alithibitisha kuwa takriban mambo yote muhimu kwa upande wa maandalizi ya kazi ya kuendesha uchaguzi huo yanakwenda vizuri kwa mujibu wa ratiba ya utekelezaji iliyoandaliwa na tume hiyo.
Aidha, aliendelea kusema kuwa, upigaji kura wa uchaguzi mdogo wa Wadi ya Chwaka utafanyika katika maeneo na vituo vilivyotumika katika Uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ambapo orodha ya wapiga kura itabandikwa katika vituo hivyo siku saba kabla ya siku ya upigaji kura.
Nao wadau wa uchaguzi wa wadi hiyo, waliiomba Tume kuendeleza jitihada zaidi ya kutoa elimu ya wapiga kura kwa wananchi wa vijijini ili kila mmoja atimize haki yake ya msingi kwani wengi wao wanaoishi vijijini hawana utamaduni wa kutumia vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii.
Uchaguzi mdogo wa Wadi ya Chwaka unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa Diwani wa Wadi hiyo, Mlenge Khatib Mlenge kilichotokea 19 Machi mwaka huu.