NA KHAMISUU ABDALLAH
SERIKALI ya mapinduzi ya Zanzibar, imesema kesi za udhalilishaji kwa mwaka 2020 pekee zilifikia matukio 1,363 yanayohusiana na ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, alitoa kauli hiyo katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Waziri huyo alisema takwimu hizo ni kwa mujibu wa ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa serikali na jeshi la Polisi Zanzibar, ambapo zinaonesha kuwa Zanzibar haipo kwenye hali nzuri na jitihada zinapaswa kuendelezwa.
Alisema katika kukabiliana na suala hilo serikali ya awamu ya nane imeanzisha mahakama maalum za kushughulikia udhalilishaji wa kijinsia kwa Unguja na Pemba na zimeshaanza kazi ili kuona kesi zinazohusiana na masuala hayo zinamalizika kwa wakati.
Alibainisha kuwa hadi Aprili 2021 takwimu zinaonesha kuwa jumla ya kesi 180 zimeshafunguliwa katika mahakama hizo, na kuamini kwamba mahakama zitatoa mchango mkubwa katika kushughulikia kesi hizo ili lengo la kupunguza na kuondoa kabisa vitendo hivyo kwa watoto na wanawake nchini liweze kufikiwa.
Kwa upande wa mahakama kuu ya Zanzibar alisema inaendelea kutekeleza jukumu lake la msingi la kutafsiri sheria, kupokea, kusikiliza na kuyatolea maamuzi mashauri yote ya jinai na madai yanayowasilishwa katika ngazi zote za mahakama ili wananchi waweze kupata haki kwa wakati.
Waziri Haruon alisema Julai 2020 hadi Machi mwaka huu mahakama hiyo imepokea na kusajili jumla ya kesi 7,507 kwa mahakama zote za Unguja na Pemba kati ya hizo kesi 4,485 zimesikilizwa na kutolewa uamuzi sawa na asilimia 60.
Alisema mahakama kuu pekee imesajili mashauri mapya 181 ambapo hadi kufikia Machi mwaka huu mashauri 17 yametolewa uamuzi sawa na asilimia 99 huku kitengo cha mahakama ya kazi kimepokea na kusajili maombi 27 ambapo hadi kufikia Machi mwaka huu tayari maombi mawili yametolewa uamuzi sawa na asilimia 7.4.
Mbali na hayo, kwa upande wa mahakama ya biashara alisema imepokea mashauri ya madai mapya matatu na kufikia mashauri 13 ambayo yapo katika hatua mbalimbali za kusikilizwa huku mahakama ya mkoa jumla ya mashauri mapya 886 yamepokelewa ambapo mashauri 97 yametolewa uamuzi hadi kufikia Machi mwaka huu.
Akizungumzia suala la kuomba na kupokea rushwa alisema matukio ya tuhuma hizo 316 yameripotiwa na kushughulikiwa katika Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar hadi kufikia Machi 2021.
Alisema makosa hayo pia ni yale ya matumizi mabaya ya ofisi, ubadhilifu wa mali na mapato, kukwepa kulipa kodi, kumdanganya muajiri, kusafirisha magendo, migongano ya maslahi, rushwa katika uchaguzi na rushwa katika zabuni.
Aidha alisema kati ya tuhuma hizo 228 zinaendelea na uchunguzi 57 zimefungwa na tuhuma 13 zimehamishiwa katika taasisi nyengine.
Waziri Haroun alibainisha kuwa tuhuma 29 zimetolewa ushauri, 13 zimefanyiwa udhibiti na tuhuma 23 uchunguzi wake umekamilika na kuwasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa ajili ya kuombewa kibali cha kuwasilishwa mahakamani na tuhuma tatu tayari zimetolewa hukumu.
Hata hivyo, alisema katika kipindi hicho jumla ya shilingi 432,585,724 zimeokolewa kutokana na operesheni mbalimbali za uchunguzi na ufuatiliaji wa makosa ya rushwa na uhujumu wa uchumi.
Alibainisha kuwa ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma katika miradi ya maendeleo nchini unaendelea ili kuhakikisha thamani halisi ya fedha kwa miradi hiyo inapatikana.
Sambamba na hayo alibainisha kuwa mamlaka hiyo inaendelea kuelimisha jamii juu ya athari na madhara ya rushwa na uhujumu uchumi kwa kufanya mikutano mbalimbali katika shehia, maskuli, ofisi za umma na binafsi na hata katika vyombo vya habari.