NA MWAJUMA JUMA

TIMU ya soka ya Uhamiaji juzi ilijiwekea mazingira mazuri ya kupanda daraja baada ya kuwafunga wapinzani wao wa karibu wanaowania nafasi hiyo Taifa ya Jang’ombe mabao 3-0.

Mchezo baina ya timu mbili hizo ambazo hadi zinashuka uwanjani hapo zilikuwa na pointi sawa, ulichezwa katika uwanja wa Amaan na kuonesha upinzani wa hali ya juu kwa pande zote mbili.

Ushindi huo wa Uhamiaji umewafikisha pointi 37 na  kuendelea kubakia kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ambayo imebakisha michezo minne kwa kila timu.

Katika mchezo huo Uhamiaji mabao yake yalifungwa na wachezaji wake Ali Haji Hassan ‘Jery’ dakika ya pili, Haji Simba dakika 49 na Said Omar Faki dakika ya 80.

Katika mchezo huo Taifa walikosa penalt iliyopigwa na Joshua Salum Bosco na kutoka nje.

Aidha katika uwanja wa Mao Zedong A kulikuwa na mchezo kati ya Mchangani United na Ngome, ambao ulimalizika kwa timu hizo kutoka sare ya kufungana mabao 2-2.