NA HASHIM KASSIM

MKUU wa kitengo cha Habari na mawasiliano wa timu ya Uhamiaji FC inayoshiriki ligi daraja la kwanza   kanda ya Unguja, Mwinyi Hamad amesema wameachana na kocha wao kutokana na mabadiliko ya uongozi katika vikosi vya ulinzi na usalama yaliyofanyika.

Alibainisha hayo wakati akizungumza na gazeti hili kwamba wameachana na benchi la lao la ufundi kwa nia njema, kutokana na makubaliano yaliyoafikiwa na pande zote mbili.

Mwinyi alisema  aliyekuwa kocha wa timu hiyo  Murtara Ahmed Kibamba ni mwajiriwa wa kikosi cha magereza, hivyo kutokana na mabadiliko ya uongozi uliotokea wameamua kusitisha mkataba wa kuinoa timu hiyo.

“Baada ya makubaliano ya pande zote mbili yaani sisi Uhamiaji FC na makocha wetu, tumeafikiana kuvunja mkataba na sababu kubwa ni kuwa kocha wetu alikuwa anatokea kikosi, na kutokana  na mabadiliko tumeamua kumrudisha nyumbani tukimuhitaji tutafuata tena taratibu” alisema Mwinyi.

Uhamiaji FC kwa sasa iko njiani kusaka kocha mpya kwa ajili ya kumalizia michezo mitano iliyobaki kukamilisha ligi hiyo, kwa mujibu wa ratiba, huku wakiwa na mchezo mmoja mkononi dhidi ya New King ambao haukuchezwa.

Licha ya kocha huyo pia timu hiyo imeachana na aliyejua kocha msaidizi Hassan Makame Ameir (Morgan), ambao kwa pamoja wameiongoza timu hiyo msimu huu kwa mafanikio na kuiacha nafasi ya pili katika ligi.

Kocha Murtara Kindamba ameiongoza timu hiyo kwa michezo 16, akishinda mechi kumi, kufungwa 3 na sare tatu pia, ligi daraja la kwanza inataraji kurejeahivi karibuni.