NA MWANDISHI WETU

UINGEREZA imesema Tanzania ni mbia muhimu wa miaka mingi wa maendeleo na katika Jumuiya ya Madola na Nchi ya Uingereza itaendelea kushirikiana katika masuala ya uwekezaji, biashara, diplomasia na utawala bora.

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika James Duddridge, ameyasema hayo katika mazungumzo rasmi aliyoyafanya na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula muda mfupi baada ya kuwasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.

Duddridge, ameongeza ziara yake ina lengo la kuendelea kuimarisha mahusiano baina ya Uingereza na Tanzania licha ya changamoto ya ugonjwa wa COVID – 19, ambapo Uingereza imekusudia kuisaidia Tanzania kuboresha mifumo ya ukusanyaji kodi, mapambano dhidi ya rushwa, lakini pia katika sekta za Afya na Elimu.

Akizungumzia ziara hiyo ya Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, amesema ziara hiyo ni kielelezo cha Tanzania kuheshimika na kukubalika miongoni mwa Jumuiya za Kimataifa na Mataifa ya nje.

Alisema kipaumbele cha Serikali ya awamu ya sita ni diplomasia ya uchumi ambapo Uingereza ni moja kati ya nchi tatu kubwa zinazowekeza hapa nchini na hivyo kuwa ni miongoni mwa Mataifa muhimu kwa Tanzania.

Balozi Mulamula, ameongeza kuwa katika mazungumzo yao msisitizo mkubwa umewekwa katika uchumi na kukuza biashara pamoja na kuiendeleza miradi mikubwa iliyokuwa ikitekelezwa na Uingereza ikiwemo miradi ya kiwanda cha sukari na madini.

Balozi Mulamula ameongeza kuwa ujio wa Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika,  James Duddridge, hapa nchini inathibitisha kuwa mahusiano ya Tanzania nje ya mipaka yake bado ni imara, licha ya taarifa potofu zilizokuwa zikisambaa katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vya nje zikitilia mashaka juu ya diplomasia ya Tanzania nje ya nchi.

Kuhusu masuala ya biashara na uwekezaji Balozi Mulamula amemuhakikishia James Duddiridge kuwa mazingira ya uwekezaji ni salama na yanavutia baada ya kuboreshwa na hivyo kumtaka kuwahamasisha wawekezaji kutoka Uingereza kuja hapa nchini kuwekeza katika sekta mbalimbali.

James kusudio la Tanzania kuendeleza mahusiano mema ya kidiploamsia na ya kiuchumi na mataifa mengine duniani na kumtaka kuhamasisha wawekezaji na wafanyabiashara nchini Uingereza kuja kuwekeza Tanzania kwa kuwa mazingira yameboreshwa.

Wakati huo huo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo na Waziri wa Uwekezaji, Geofrrey Mwambe wamekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo ya Uingereza, James Duddridge.

Kikao hicho Mawaziri hao wamepata fursa ya kujadili masuala mbalimbali ya kudumisha na kukuza mahusiano ya biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza hususani kwa bidhaa muhimu za Tanzania kuuzwa nchini Uingereza na kuvutia  Uwekezaji mkubwa wa Uingereza hapa nchini.

Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Katibu Mkuu,  Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Prof. Godius Kahyarara pamoja na Balozi wa  Uingereza nchini Tanzania, David Concar.