ZASPOTI

MICHEZO ni burdani inayopendwa na watu wengi duniani ikiwa kwa kucheza au kutizama.
Tumeshuhudia katika nchi mbali mbali duniani jamii hupendelea michezo na hata wale washiriki wa michezo aina mbali mbali hupata umaarufu na hata kutajirika.

Miongoni mwa nchi ambazo zimekua mstari wa mbele kupenda michezo ni Zanzibar, ambapo wananchi wake wengi hushiriki katika michezo aina mbali mbali.
Kutokana na umuhimu wa michezo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeliona hilo na kuunda wizara ambayo inashughulika na sekta hiyo.

Kuwepo kwa wizara hiyo kunasaidia umuhimu wa michezo na kuondosha changamoto mbali mbali ambazo zinaikabili sekta hiyo.
Mapema mwezi Januari mwaka huu visiwa vya Unguja vilirindima kwa mashindano ya kuwania kombe la Mapinduzi. Mashindano hayo ambayo yalifanyika katika uwanja wa Amaan na kujaza mashabiki wengi ambao kwa lengo moja kuja kuangalia burudani.

Mashindano hayo ambayo yalichukua takriban siku nane na mashabiki kutoka maeneo mbali mbali ya Tanzania walishiriki hususan siku ya fainali baina ya Simba na Yanga.
Kilichojitokeza siku ya fainali ya mtanange huo ni kujaa kwa uwanja ambapo hata nafasi za kukaa zilikosekana kutokana na mashabiki wengi kutaka kushuhudia.

Lakini pia hata mashabiki wengi walishindwa kuingia kiwanjani hapo na kulazimika kupiga kelele za malalamiko zilizoonesha kukerwa kwao kwa kukosa kuingia kwenye majukwaa na kuona mchezo huo.
Mbali na mashabiki, lakini, hata wanahabari ambao nao ndio walikua mstari wa mbele kuyatangaza mashindano hayo walikosa sehemu ya kukaa na kulazimika kukaa kwenye tatani za uwanja huo.

Tulichokigundua ni kuwepo kwa udogo wa uwanja huo ambao kwa njia moja au nyengine unahitaji kuongezwa ili fursa kama hizo zinapotokea wananchi waweze kushuhudia.
Kwa hapa Unguja vipo viwanja viwili maarufu vya soka ikiwemo kiwanja cha Amaan na kile cha Mao Zedong, lakini, kutokana na Amaan ni uwanja unaotambulika kuchezwa mechi za kimataifa hivi sasa hautoshi kutokana na idadi kubwa ya waangaliaji wa mashindano makubwa kama Kombe la Mapinduzi.

Kwa mujibu wa tathmini inaonesha kwamba uwanja wa Amaan una uwezo wa kuchukua mashabiki 12,000 wakati uwanja wa Gombani una uwezo wa kuchukua watu 40,000.
Tukiangalia idadi ya watazamaji ya uwanja wa Amaan ni ndogo kwani hata wale walioingia siku ya fainali ya Mapinduzi walipitiliza idadi hiyo, hivyo, itakuwa jambo la busara kwa Serikali ya Awamu ya Nane kuhakikisha inafanya bidii ya kutafuta eneo ambalo litakidhi haja ya kujenga uwanja mwengine.

Tunaamini kama kutajengwa uwanja mwengine utakaokuwa mkubwa na wa kisasa utaingiza mashabiki wengi na pia kuiingizia mapato mengi serikali.

Katika kisiwa cha Unguja yapo maeneo mengi ya wazi ambayo yanaweza kutumika kujenga uwanja ambao utasaidia kukidhi haja, lakini, kama kutokosekana eneo la kujengwa kwa uwanja huo, ni vyema serikali kutafuta wataalamu na kutumie maeneo yalio wazi ili kuutanua uwanja zaidi.
Ni imani yetu kwamba serikali yetu ya awamu ya nane chini ya uongozi wa Dk. Hussein Mwinyi utalifanyia bidii ili kukihidhi haja ya mashabiki wa michezo hasa soka kwenye uwanja huo.
Zanzibar yenye neema ya michezo inawezekana.