NEW YORK, MAREKANI
BARAZA la usalama la Umoja wa Mataifa litakutana wakati wowote kuanzia sasa katika kikao cha dharura kuhusu mgogoro wa ghasia zinazoongezeka Jerusalem.
Hayo yameelezwa na gazeti la Times la Israel ambalo limewanukuu wanadiplomasia wa nchi hiyo.
Kikao cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kitafanyika kwenye faragha baada ya Tunisia kutoa ombi la kuitishwa kikao hicho.
Katika siku chache zilizopita makabiliano yameongezeka ambapo leo wapalestina zaidi ya 300 walijeruhiwa baada ya kushambuliwa na polisi wa Israel katika eneo takatifu la Jerusalem uliko msikiti wa Al-Aqsa.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameitaka Israel kujizuia na matumizi ya nguvu.
Aidha jeshi la Israel jan limefahamisha kwamba linasitisha kwa siku moja operesheni yake kubwa ya mazowezi ambayo hayajawahi kufanyika kwa kipindi cha miaka 30, ili kuelekeza juhudi zote katika maandalizi ya uwezekano wa kutokea machafuko wakati mvutano ukiongezeka na Wapalestina katika eneo hilo la Jerusalem.