NA LAYLAT KHALFAN

MSTAHIKI Meya wa Jiji la Zanzibar, Mahmoud Mohamed Mussa, amesema jiji limeandaa mkakati wa utekelezaji wa usafi kama ilivyoagizwa na serikali kuu.

Aliyasema hayo alipokuwa akifungua kikao cha bajeti cha baraza hilo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 na mwaka 2020 /2022 ofisini kwake Forodhani mjini Zanzibar.

Alisema suala la usafi limepewa kipaombele katika masoko na maeneo mbalimbali ya mji wa Zanzibar, lakini bado linaeonekana ni la kusua sua.

Alisema serikali kuu bado haijaridhishwa na hali ya usafi katika mkoa wa mjini Magharib, hivyo aliwataka Madiwani  kulisimamia vyema jukumu hilo, ili lengo la serikali liweze kufikiwa.

“Nitahakikisha Zanzibar inakuwa safi na salama hususan kwa mkoa huu kwani ndio kitovu kiuu cha wageni wanaoingia nchini”, alisema.

Akizungumzia kuhusu mapato, Mahmoud alisema ipo haja kwa mabaraza kujipanga upya ndani ya Manispaa zao kwani hali ya makusanyo bado hairidhish  na alizitaka kuhakikisha wanatoa risiti za kielektroniki kwa watu wanaotaka huduma, ili kudhibiti uvujaji wa mapato.

Akiwasilisha bajeti ya makadirio ya matumizi kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kwa niaba ya Mkurugenzi, Ofisa Mipango wa Jiji hilo, Ghanima Haji Sheha, alisema ili jiji kuliwezesha kiuchumi limeanza mpango mkakati kibiashara ili kuwezesha kuendelea na hatua ya kufanya miradi ya kiuchumi na maendeleo.

Aidha, alisema tayari jiji limeimarisha mashirikiano na wadau wa ndani na nje katika kuleta maendeleo jijini humo sambamba na kubuni na kuanzisha vyanzo vya mapato vya baraza la jiji hilo.

Katika kuandaa mikakati hiyo, jiji limeomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi 1,115,700,000, kati ya fedha hizo shilingi 825,500,000 kwa kazi za kawaida na shilingi 290,200,000 kwa ajili ya mishahara kwa mwaka wa fedha 2021\2022.