NA MWAJUMA JUMA

WATENDAJI wa vyombo vya habari wameshauriwa kuweka mikakati madhubuti katika sehemu zao za kazi ili kuleta usawa wa kijinsia na kuondokana na udhalilishaji.

Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA Zanzibar) Dk. Mzuri Issa, alipokuwa akitoa mada kuhusu mapungufu ya kijinsia katika uhuru wa kujieleza katika vyombo vya habari Zabzibar.

Mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao, ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Habari Duniani (WPFD), uliandaliwa nan a Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Zanzibar na shirika la Internews kwa njia ya mtandao.

“Tunapaswa kuweka mifumo na taratibu za kukabiliana na usawa wa kijinsia kwa kuweka sera na miongozo ya kijinsia ambayo itasaidia kuweza kuona mapungufu yaliyomo na kuweza kufanyiwa kazi,” alisema.

Alieleza kuwa katika kufikia huko waandishi na wao wanatakiwa kuwajibika kwa kuonesha mapungufu yatakayoonekana na kuyawekea utaratibu wa kupambana nayo.

Sambamba na hayo aliwataka waandishi wa habari wanawake kutoona aibu kuripoti madhila na unyanyasaji wa kijinisa wanayofanyiwa katika sehemu zao kazi.

Akiwasilisha mada ya changamoto za vyombo vya habari, Mwandishi Mwandamizi, Rashid Omar Kombo, aliwataka waandishi wa habari kuwa kufanya kazi zao kwa kujitolea, kuwa wazalendo na kutoogopa ili kuongeza kasi ya maendeleo ya nchi.

“Habari ni bidhaa muhimu inayohitajiwa na jamii kwa kuwa inatoa mwanga kwa jamii kuelewa kile ambacho serikali inafanya lakini pia kutambua wajibu na hatua za kuchukua,” alieleza Kombo.

Awali akiwasilisha mada ya uhuru wa vyombo vya habari Zanzibar kwa mtazamo wa sheria, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC), Harusi Miraji Mpatani, alisema kuwa uhuru wa kujieleza ni msingi muhimu katika uhifadhi na utekelezaji wa haki za binadanu.

Alieleza kuwa iwapo uhuru wa habari utaminywa, kutawafanya watu washindwe kujitetea hivyo ipo haja kwa mamlaka kuzingatia katiba na sheria wanapotekeleza majukumu myao.

“Mnaweza kutumia vikao na njia mbali mbali za kuhamasisha marekebisho ya sheria ili kuhimiza uwepo wa uhuru wa habari ili muweze kufanya kazi zenu kwa ufanishi zaidi,” alieleza mpatani.

Kwa upande wake meneja mipango wa Internews, Shaabani Maganga, aliwapongeza wanahabari wa Zanzibar kwa kushiriki kikamilifu na kutoa maoni ambayo yatawezesha kuchukuliwa kwa hatua zaidi za ulinzi na uhifadhi wa haki na uhuru wa habari.

“Niwapongeze nyote kwa kushiriki vyema, niwashauri kutumia vyema fursa iliyotolewa na serikali iliyopo ambayo kwa kiasi kikubwa inaonesha utayari wa kutanua wigo na uhuru wa habari Zanzibar,” alieleza Maganga.

Katika mkutano huo, washiriki walitumia fursa hiyo kutoa maoni yao juu ya mambo mbali mbali yanayohusiana na tasnia ya habari ikiwa ni mwendelezo wa mikutano ya wadau kuelekea kilele cha maadhimisho hayo kitaifa yatakayofanyika Mei 23 mwaka huu.