NA ALLY HASSAN, DOMECO
WAFANYABIASHARA wa Chakula na vitu vya kuchezea, wamesema hali ya biashara katika Skukuu ya mwaka huu zimenda vizuri tofauti na miaka iliyopita.
Wakizungumza na Zanzibar Leo, katika viwanja vya skukuu vya Mnazimmoja Mjini Unguja, walisema kuna changamoto ndogo ndogo walikumbana nazo, iwapo zitashughulikiwa kwa wakati wataweza kunufaika zaidi pamoja na kukuza pato la nchi.
Rahma Abdallah Ali, ambaye ni Mwenyekiti na muuzaji wa vitu vya kuchezea, alisema kuna tofauti kubwa ya kibiashara katika siku kuu ya Edd el-Fitri ya mwaka huu na miaka mengine iliopita kutokana na kuongezeka kwa watu wengi na wanunuzi wa bidhaa hio.
Aidha, alisema ucheleweshwaji wa kutolewa mabanda ya kufanyia biashara katika eneo hilo limekuwa ni kikwazo kikubwa kwao ambacho kinawafanya wachelewe kuweka bidhaa zao mapema sambamba na uzimwaji wa taa mapema.
“Tunauomba uongozi utuongezee muda kutoka saa nne angalau hadi saa tano za usiku katika siku kuuu zijazo kutokana na watu wengi wanatoka sehemu za mbali tukizingatia bara barani kuna foleni za magari, ambazo zinawafanya wanachelewa kufika hapa na kuwafanya wanatembea kidogo tu muda unaisha na umeme unazimwa,” alisema.
Rahma alisema changamoto nyengine ni uchache wa vyoo katika eneo hilo, limekuwa ni mwiba kwao wafanyabiasha na watu wote ambao wanatumia vyoo hivo, amewaomba wahusika wanao simamia suala hilo kuwajengea vyoo vyengine au kuwawekea vyoo vya muda (kuhamishika) ambavyo walikuwa wakitumia sikukuu zilizopita ili kupunguza msongamano katika vyoo vilivyokuwepo.
Nae Hakim Ame Mbuki, mfanyabiashara wa chakula katika eneo hilo, alisema biashara yake imekwenda vizuri ila wamekosa huduma ya maji imewafanya watoke eneo hilo na kwenda kwengine kutafuta huduma hiyo, ili kufanya biashara zao katika mazingira mazuri.
“Wito wangu kwa serekali kwa sisi wafanya biashara wa vyakula tunahitaji sana maji, tunawaomba watutengenezee mabomba ya maji au mbadala wake japo watuletee magari ambayo yataleta maji ili tuweze kufanya biashara zetu vizuri,” alieleza Hakimu.
Mhasibu Mapato wa Manispaa ya Mjini ambaye ni Msimamizi wa kiwanja hicho, Mohammed Tahir Mohammed, alisema ugawaji wa mabanda katika kiwanja hicho haujacheleweshwa isipokuwa kuna baadhi ya wafanya biashara hawakufuata taratibu za malipo mapema katika ofisi za Manispa hiyo ambazo zimewafanya wachelewe kupewa mabanda hayo.
Aliema suala hilo, alilisimamia yeye mwenyewe toka ulipofika mwezi 28, Ramadhani, walianza kugawa mabanda hayo na alihakikisha watu wote walio fuata taratibu za malipo wanakabidhiwa mabanda hayo kabla ya yeye kuondoka katika viwanja hivyo.
Aidha aliwataka wafanyabiashara wanaotaka kutumia viwanja kipindi cha skukuu kufika mapema kwa uongozi wa Baraza hilo, ili waweze kufuata taratibu zote zinazotolewa na viongozi wa juu ikwemo Mkuu wa Mkoa.
Mohammed alisema uwepo wa vyoo vichache katika viwanja hivyo ni kweli ila mara nyingi huwa wanatumia vyoo vya kuhamishika, ila kwa mwaka huu ilikuwa ni tofauti kutokana na kutokuwanavyo wao na kupelekea kwenda kukodi sehemu nyengine.
Alisema suala la umeme na maji yanaendelea kushughulikiwa sambamba na changamoto nyengine, ili siku kuu za miaka mengine kuondokana na kadhia zilizojitokeza katika kipindi cha siku kuu zilizo pita.