NA MWANAJUMA MMANGA
WANANCHI wa Zanzibar wametakiwa kufuga nyuki kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kuepusha kuzalisha biashara zitazoleta madhara kwa mtumiaji.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya wafuga nyuki Zanzibar (ZABA) Salum Khamis Juma, aliyasema hayo huko Kitogani Wilaya ya Kati, mkoa wa Kusini Unguja katika kilele cha siku ya nyuki duniani mei 20, mwaka huu.
Alisema iwapo wazalishaji wa mazao ya nyuki watazingatia njia za kisasa, watapunguza hatari na madhara kukosekana kwa soko la bidhaa hizo kwa nchi za Afrika.
“Mfano wa mazao kama matikiti na tungule hutumia sana dawa na mbolea zenye kemikali ambayo yanaathiri afya za walaji jambo linalopelekea kupunguza wateja,” alieleza.
Aidha alisema kumekuwa na changamoto ya uharibifu wa misitu hasa ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa hali ambayo inasababisha upatikanaji wa asali.
Aliongeza kusema kuwa changamoto nyengine ni ukosefu wa upatikanaji wa vifaa vya kufugia pamoja na vifungashio hali ambayo inapelekea kuvifata Tanzania bara na kusuasua kwa soko hapa Zanzibar.
Hivyo ameiomba serikali na Wizara husika kusaidia upatikanaji wa vifaa hivyo ili wakulima kutokata tamaa na kufikia malengo yao.
Hata hivyo aliwataka wananchi kufuga nyuki kibiashara kwani wataweza kupata soko la uhakika na kuingia katika ushindani wa kibiashara.
Alisema wanapofuga nyuki kwa uhakika wananchi hao wataweza kupata kipato cha mtu mmoja mmoja na kuleta tija kwao na taifa kwa ujumla.
Alisema changamoto nyengine wizi wa asali na utiaji wa moto katika maeneo ya misitu jambo linalowaathiri kwa kiasi kikubwa wanachama wao.
Naye Katibu wa Jumuiya hiyo, Abdi Burhani Abdalla, alisema malengo ya jumuiya hiyo ni kuwafanya wanajumuiya hiyo kuwa na sauti moja ili kusaidia wakulima kuwa na elimu ya kibiashara na upatikanaji wa soko bidhaa wanazozalisha.
Alisema siku hii huadhimisha kwa usafi na kongamano la utoaji wa elimu ya nyuki ambapo nyuki katika chakula wanatoa asilimia 90 na robo 3 katika chakula cha nyuki.
Alifahamisha kuwa bado kuna ukakasi wa utoaji wa takwimu kwa wafugaji hivyo ni vyema kuweka takwimu hizo kwa faida ya serikali.
Alisema malengo ya baadae katika jumuiya ni kufuga nyuki kibiashara ili kuufikia uchumi wa buluu, pia kuwa na sauti moja pamoja na serikali kuunda sera ya nyuki ili nyuki wasibughudhiwe.
Mmoja ya wakulima aliyefaidika na shughuli za ufugaji wa nyuki, Mwanajuma Mahadhi Mussa, alisema amepata faida kubwa katika kilimo hicho kwani kimeweza kumletea maendeleo kwake na kwa familia.
Alisema faida moja anaoipata ameweza kuzalisha na kupata asali katika mizinga 20 na anatoa asali lita tano, pia amezalisha sabuni, shampuu, hivyo amewataka wanawake wenzake kujikita zaidi kufuga nyuki kwa maendeleo kwani wanaweza kujikomboa na ajira.
Jumuiya ya ZABA ilianzishwa rasmi mwaka 2000 na kusajiliwa mwaka 2002 ambapo kwa sasa ina wanachama katika vikundi 42 unguja na wanachama 15 waliadhimisha siku hiyo kwa kongamano na usafi wa mazingira ili kujenga uelewa wa jamii juu ya umuhimu wa nyuki na mazao yake.