KAMPALA, UGANDA

WANANCHI wa Uganda wamekuwa na mawazo tofauti baada ya rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni hapo juzi kuapishwa kuiongoza nchi hiyo kwa awamu ya sita

Kwa mujibu wa wanaomuunga mkono Museveni aendelee kuwa rais wa nchi hiyo wamebainisha kuwa utawala wake umeliweka taifa hilo kwenye utulivu na kuwepo amani.

Wananchi hao wanaomuunga mkono rais huyo walibainisha kuwa utawala wa Museveni umeondosha mapinduzi ya kijeshi ya mara kwa mara yaliyokuwa yakitokea nchini humo na kuliweka taifa hilo katika taharuki.

Hata hivyo kwa upande wa pili wa shilingi, wale wanaompinga rais huyo wanasema kuwa anaongoza nchi hiyo kwa mabavu bila ya kuzingatia misingi ya utawala wa sheria.

Watu hao wanaompinga wanasema kuwa ameshindwa kusimamisha demokrasia, anaminya uhuru wa habari na vyombo vya usalama nchini humo vinatumika vibaya dhidi ya raia hasa wapinzani.

Wakati huo huo, rais huyo alimewaomba viongozi wa Afrika wenye kuhitilafiana kuungana katika nyanja mbalimbali zikiwemo za ulinzi hali itakayosaidia Afrika kuondoka na migogoro.

Akizungumza mara baada ya kuapishwa, Museveni alisema migogoro katika nchi kama vile Libya, Afrika Kati, Somalia na Msumbuji inaweza kutatuliwa kama nchi za Afrika zitaongeza ushirikiano.