NA MARYAM HASSAN

MAHAKAMA kuu iliyopo Vuga mjini Zanzibar, imetupilia mbali ombi la upande wa utetezi juu ya kupewa dhamana wakurugenzi wa kampuni ya ‘Master Life Microfinance Limited’.

Maamuzi hayo yalitolewa na Jaji wa mahakama kuu Zanzibar, Aziza Iddi Suwedi, baada ya kujiridhisha na hoja zilizotolewa na upande wa mashitaka wa serikali.

Jaji Aziza alisema hoja zilizotolewa na upande wa serikali zimekubalika, kwamba sheria ambayo upande wa utetezi walikuwa wanaipinga inaweza kufanya kazi na inaendana na muda uliofikishwa kosa husika.

Awali mawakili hao waliwaombea wateja wao kupewa dhamana lakini upande wa mashitaka ulipinga jambo ambalo lilisababisha kesi hiyo kuahirishwa ambapo Mei 27 mwaka huu ilikuwa katika hatua ya kutolewa maamuzi.

Mawakili hao walitaka sheria hiyo ianze mara tu baada ya kusainiwa na Rais Mwinyi bali Jaji huyo alieleza kwamba sheria hiyo inarudi nyuma, ambapo itawagusa mpaka wale wote waliotenda makosa nyuma ikiwemo waliyoshitakiwa nayo wateja wao.

Itakumbukwa kwamba miongoni mwa makosa yanayowakabili ikiwemo kukwepa kodi na utakatishaji fedha hayana dhamana kwa mujibu wa sheria nambari 1 ya mwaka 2021, ambayo ilisainiwa Machi 8 mwaka huu na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Baada ya kutolewa maamuzi hayo mawakili ambao walikuwa wanawatetea wakurugenzi hao wa ‘Master Life’, wameamua kujitoa jambo lililosababisha hofu.

Waliojitoa katika kesi hiyo ni Hassan Kijogoo na mwenziwe kabla kesi hiyo haijatolewa maamuzi na Jaji Aziza.

Nje ya mahakama Zanzibar Leo lilizungumza na Hassan Kijogoo alisema wameamua kujitoa baada ya kukosa maelekezo na kiongozi mkuu wa ‘Master Life’ ambae yupo nje ya nchi.

“Huyu ndiye anayelipia huduma za sheria kwa wateja wake ambao sisi tutawawakilisha lakini hakuna mashirikiano hivyo tumeamua kujitoa”, alisema Kijogoo.

Katika kesi hiyo amebaki wakili Said Mayungwa na Rashid Abdalla ambae anawasimamia wakurugenzi hao kwa muda uliobaki na kuahidi kuwapigania.

Aidha kwa upande wa Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka ambao wameisimamia kesi hiyo ni Mohammed Saleh (DPP) Mohammed Kombo mawakili waandamizi.

Wakurugenzi hao ni Mzee Said Hassan (29), Joseph Alban Mwale (32, Abudu Abdalla Haji (31), Muslim Jaffar Abdul-rasul (54) na Kassim Abdi Kassim (33).

Kesi imeahirishwa wa washitakiwa hao wamerudishwa rumande hadi Julai 1 mwaka huu kesi yao itapoanza kutajwa.