NA HAJI NASSOR

WANANCHI wanaoishi nyumba za maendeleo Kengeja wilaya ya Mkoani Pemba, wamesema hawakatai agizo la serikali la kuhama katika nyumba hizo kwa sababu ya uchakavu, lakini hawajui sehemu ya kwenda.

Walisema, umaskini wa kipato walionao ndio uliosababisha nyumba hizo kuchakaa, hivyo walisema wanahitaji kupewa makazi na serikali ili wahame.

Wakizungumza na waandishi wa habari kijijini hapo, walisema kutokana na hali zao za kipato, wanashindwa kuzitengeneza nyumba hizo, hivyo ni vyema serikali ikaingilia kati.

Walisema, wanathamini na kuheshimu mno agizo ililotolewa na serikali ya kuwataka hawahame lakini kwa sasa hawajui eneo gani wahamie.

Mmoja kati ya wananchi hao, Mohamed Said Machano, alisema anaishi katika nyumba hizo kwa zaidi ya miaka 40 sasa na akitolewa hapo hajui akahamie wapi na familia yake.

Alikiri kuwa, amepokea barua kutoka serikalini ikimtaka ahame na hapingani na agizo hilo lakini bado hajajua wapi akahamie.

Nae Mohamed Jafu Khamis alisema alihamia ndani ya nyumba hiyo akiwa na wazee wake tokea mwaka 1977, ambapo miaka 15 iliyopita baada ya nyumba hizo za ghorofa kuvuja, walipeleka kilio serikalini.

Alieleza kuwa, baada ya hapo idara ya majenzi ilipeleka bati 1,000 kwa ajili ya kuezeka lakini baada ya muda walizotoa na kuiacha nyumba hizo zikivuja.

“Tatizo la uchakavu wa nyumba hizi ni kutokana na kupenya maji yanayotuama varanda, kwani hayana miundombinu ya kumwagika chini,” alisema.

Asha Makame Kombo, alisema ataendelea kubakia ndani ya nyumba hiyo hadi pale serikali itakapompatia eneo jengine la kuishi.

“Ni kweli taarifa za kunitaka kuhama ndani ya nyumba hii ninayo, lakini najiuliza niende wapi kwa sababu hapa ninaishi zaidi ya miaka 40, ndio kwetu sina pengine,”alieleza.

Alieleza kuwa, ni kweli wenzake wamehama kwa sababu wana maeneo mengine ya kwenda, lakini yeye alitegemea hapo, hivyo kama kuna amri ya kuhama kwanza atengewe eneo la kujihifadhi.

Kwa upande wake, Mtumwa Khamis Juma, alisema hana mpango wa kuhama kwa sasa.

Juma Khamis Ali, alisema ingawa wazazi wake wamefariki na kumuachia nyumba hiyo ya urithi, hajui wapi akaishi kwani walikondolewa na serikali, sasa kuna makaazi ya askari wa magereza.

Vuia Kheir Vuai na Ali Khamis Kheir 80, walisema kama serikali inawataka wahame, kwanza wawatengee maeneo ya kijihifadhi na familia zao.

Walimuomba Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kuwatembelea, ili kuona hali zao.

Walisema, nyumba hizo za ghorofa ni moja ya matunda ya mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, ambazo ziliasisiwa na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, hivyo ni vyema zikaendelezwa.

Sheha wa shehia ya Kengeja, Mohamed Kassim, alikiri kupokea nakala ya barua hiyo, ambayo inawataka wananchi wake kuhama katika nyumba hizo.

Aprili 6, mwaka huu wananchi 27 wanaoishi katika nyumba hizo, walipokea taarifa ya kutakiwa kuhama kutokana na uchakavu wa nyumba hizo.

Barua hiyo yenye kumbu kumbu namba EA.133/172/01/46 imesainiwa na Ofisa Mdhamini wa Wizara ya Ardhi, Maendeleo ya Makaazi.

Sehemu ya barua hiyo, imewataka wananchi hao kuhama kwa sababu nyumba hizo hazina  huduma za kibinadamu kama vile maji safi na salama na uchakavu.

Nyumba hizo zina uwezo wa kuishi familia 48, na tayari famila 27 zimehama.

Wananchi hao walikabidhiwa nyumba hizo kama fidia, baada ya kuhamishwa katika makaazi yao ya asili eneo la Makomba shehia ya Kengeja, ili kupisha ujenzi wa chuo cha mafunzo na nyumba za askari, na kukabidhiwa na rais wa awamu ya pili, marehemu Aboud Jumbe Mwinyi.