NAYPYITAW, MYANMAR
VIFO vinavyotokana na mashambulizi ya jeshi la Myanmar dhidi ya waandamanaji wanaopinga hatua ya jeshi la nchi hiyo ya kutwaa madaraka kinyume cha sheria imeongezeka na kupindukia 800.
Katika ripoti ya kila siku iliyochapishwa na Shirika la Misaada la Wafungwa wa Kisiasa (AAPP), imeelezwa kuwa, watu 6 zaidi wamefariki dunia katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita nchini Myanmar na kuifanya idadi ya watu walioaga dunia hadi sasa kufikia 802.
Ripoti zaidi zinasema kuwa, zaidi ya watu 4000 wametiwa mbaroni na wanashikiliwa na vyombo vya usalama vya Myanmar.
Pamoja na ukandamizaji huo wa jeshi, wananchi wa Myanmar wanasisitiza kuwa, wataendelea kuandamana hadi pale takwa lao ambalo ni kuacha demokrasia ichukue mkondo wake litakapoheshimiwa na kutekelezwa.
Maandamano ya wananchi hao sasa yameingia katika mwezi wake wa nne tangu yalipoanza mwezi Februari kupinga hatua ya kijeshi ya kutwaa madaraka ya nchi hiyo kinyume cha sheria.
Jeshi la Myanmar lilitwaa madaraka ya nchi Februari Mosi mwaka huu baada ya kumkamata Rais wa nchi hiyo, Win Myint na viongozi wengine akiwemo Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama tawala mwenye ushawishi mkubwa, kufuatia siku kadhaa za mivutano nchini humo.
Kisingizio cha jeshi cha kufanya mapinduzi hayo ni madai yake ya kutokea wizi na udanganyifu katika zoezi la uchaguzi wa Bunge wa Novemba mwaka jana (2020), ambapo kwa mujibu wa matokeo, chama tawala cha National League for Democracy (NLD) kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi kiliibuka na ushindi.