NA  BAKAR MUSSA, PEMBA

WANAFUNZI wa Chuo kikuu cha Taifa ( SUZA)  Kampasi ya Benjamin Mkapa Pemba, wametakiwa kumuunga mkono Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,  Dk. Hussein Ali Mwinyi , kwa ajili ya Ukusanyaji wa kodi kwa kuwa na utamaduni wa kudai risiti pale wanapofanya manunuzi.

Akizungumza na wanafunzi hao huko katika ukumbi wa Chuo hicho ulioko Mchangamdogo Pemba, Ofisa uhusiano wa Bodi ya mapato Zanzibar (ZRB), Makame Khamis Moh’d, alisema Serikali imepiga hatuwa kubwa katika ukusanyaji wa mapato jambo ambalo limepelekea kutekeleza baadhi ya mambo yake kwa fedha zake wenyewe.

Alieleza pamoja na mafanikio hayo lakini bado juhudi zaidi zinahitajika kuchukuliwa na wananchi mbali mbali, ikiwemo Wanafunzi wa Vyuo kuwahamasisha wengine kudai na kutowa risiti, pale wanapofanya mauzo ili kudhibiti uvujaji wa mapato .

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inalengo ya kuwaletea maendeleo ya haraka wananchi wake ikiwemo ya Elimu na sekta nyengine muhimu , lakini ili kufikia malengo hayo ni lazima kuwe na udhibiti wa mapato kwa kuona kila mmoja ni jambo linalomuhusu.

Ofisa uhusiano  kutoka Bodi ya mapato Zanzibar (ZRB) Badria Massoud Attai, aliwataka wanafunzi hao kuelewa kuwa kila nyaraka inayotolewa na Serikali huwa inalipiwa kodi kama vile vyeti vya kuzaliwa, ununuzi wa mafuta, tiketi za usafiri wa aina yoyote hivyo wasiwe tayari kukataa risiti pale wanapokwenda kutafuta nyaraka hizo.

Alisema  mwananchi kuwa na risiti kwa bidhaa alionunua  inaipa uhalali na umiliki wa bidhaa hiyo, kwani risiti yoyote inayotolewa imetengenezwa kisheria na inanembo yake ya Serikali.

Alifahamaisha ni kosa kwa mfanyabiashara kufanya shuhuli za kibiashara katika eneo lolote la Zanzibar bila kujisajili kwa mamlaka husika juu ya biashara anayoifanya na kujuilikana kwa lengo la Serikali kupata mapato yake.

Nae Raya Suleiman Abdalla, Ofisa uhusiano wa ZRB Zanzibar, alisema ulipaji kodi ni suala muhimu na la kisheria, hivyo kila mmoja anawajibu wa kulisimamia hilo ikiwa ndio njia ya kujipatia maendeleo yao ya haraka.