NA MARYAM HASSAN, TUWERA JUMA(MCC)
WIZARA ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, imesema hakutakuwa na uhakika wa ajira kwa vijana ambao wanajitolea wa ujenzi wa Taifa.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Wizara hiyo, Masoud Ali Mohammed, wakati akijibu suali la msingi lililoulizwa na Mwakilishi wa Wanawake, Fatma Ramadhan Mandoba, aliyetaka kujua serikali inampango gani wa kuwapatia ajira wale wote waliomaliza mafunzo ya kujitolea JKU.
Waziri huyo, alisema vijana hao mara baada ya kumaliza mafunzo hupatiwa cheti, ambacho kitamuwezesha kutafuta ajira sehemu yoyote pale fursa inapotokezea katika taasisi za serikali au binafsi pamoja na kujiajiri mwenywewe.
Aidha, alisema kwamba suala la ujenzi wa Taifa kwa kijana pia ni njia ya kumjengea uwezo, ili aweze kujitegemea.
“ Napale fursa za ajira zitakapopatikana serikalini na wao wataangaliwa kwa mujibu wa sheria za uajiri katika vyombo hivyo” alisema Waziri huyo.
Aidha aliongeza kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 14 (1) cha sheria ya JKU ya mwaka 2003 pamoja na kifungu 163 (1) (a) na (b) kanuni ya JKU 2010 ni miaka miwili wanapatiwa mafunzo vijana walio maliza elimu ya lazima ya kidato cha nne , na mwaka mmoja waliomaliza kidatu cha sita.
Alisema kila kijana ambae atatumikia JKU kwa Ujenzi wa Taifa mara baada ya kumaliza Ujenzi wake atatunukiwa cheti maalum.
Katika suala la nyongeza, Mwakilishi huyo pia alitaka kujua Serikali inamikakati gani kuwapatia ajira vijana waliotumikia miaka miwili na kuacha kuwapa ajira wale ambao hawajatumikia JKU.
Alisema hiyo ni changamoto kubwa kuajiri vijana ambao hawajatumikia katika Ujenzi wa Taifa , hivyo serikali imesema italifanyia kazi suala hilo.
Azza Januari Joseph, alitaka kujua mfuko wa uwezeshaji unawawezesha vipi vijana katika kuwapatia mikopo, ili waweze kujiari wenyewe kwa vijana waliotoka JKU.
Alisema Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Uwezeshaji wanahakikisha kuwa mfuko huo unawawezesha vijana wote bila ya kujali kuwa wamepita JKU au la .
Hivyo aliwataka vijana kuutumia mfuko huo, ili kujinufaisha kiuchumi na kujiendeleza kwa ajili ya kupata kipato.