TEKNOLOJIA ya habari na mawasiliano imekuja na mchango wa kipekee katika kuwawezesha wananchi kupata taarifa muhimu wanazozihitaji na kuzipata kwa wakati muafaka ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla ya kuibuliwa kwa teknolojia hiyo.

Maendeleo haya yamekuwa chachu ya kuiwezesha jamii kujua mambo mbalimbali katika nyanja za kukuza uchumi, mambo ya kijamii, maisha ya kisiasa na kadhalika.

Kupitia mitandao hiyo lolote linalofanyika duniani kwa umbali wowote, tunaweza kuliona kwa muda mfupi sana na hata kuweza kuliona moja kwa moja wakati tukio likitokea.

Ni ukweli uliowazi kwamba mtu wenye taarifa nyingi na sahihi zaidi juu ya masuala mbalimbali ndio wenye nafasi bora zaidi ya kufanya maamuzi sahihi, hivyo mitandao ya kijamii ni darasa tosha la kutoa uelewa na kumsaidia mtu kufanya maamuzi.

Kutokana na hali hiyo ndipo hapa panapobainisha kuonekana umuhimu wa kipekee wa vyombo vya habari kwenye masuala mbalimbali katika kijamii.

Tunakumbuka vyema kabla ya matumizi ya intaneti kushamiri njia kuu tulizokuwa tumezizoea kwa ajili ya kupata taarifa za masuala tafauti ni kupitia vyombo vya habari vya kizamani ambavyo hadi leo vimekuwa vikitumika na vinaendele kwa muhimu.

Tuseme wazi kabisa kwamba, licha ya faida nyingi za mitandao ya kijamii tunazoziona hivi sasa ikiwemo kupata habari nyingi na kwa urahisi zaidi popote ulipo, kwa upande mwengine kuja kwake kumetuletea changamoto kubwa.

Tulidhali vijana wanaweza kuitumia mitandao hiyo kuongeza elimu kutokana na masomo yao, kwa mfano kuangalia vitabu na maelezo mbalimbali ya wataalamu walioelezea juu ya mada ya somo fulani.

Tofauti na makusudio ya matumizi ya mitandao ya kijamii ilivyokusudiwa, mitandao hiyo imekuwa chanzo kikubwa cha uvunjifu wa maadili katika jamii hasa kwa vijana.

Kupitia mitandao hiyo, vijana wamekuwa wakijifuza yasiyowahusu na hivyo kuyafanyia majaribio mitaani, ndio maana hatushangai sana maovu na machafu yameenea ikiwemo ubakaji na ulawiti.

Mitandao hiyo imekuwa ukumbi wa wengine kuwafundisha maovu wengine, huku wengine wakiitumia kwa kusutana na hata kutukanana bila ya hata kubakishana.

Kibaya zaidi wale wagonjwa wa siasa nao hawako nyuma wanaitumia mitandao hiyo kwa kuwatukana na kuwakashifu viongozi wetu, bila sababu yoyote.

Wakati mwengine mpaka tunajiuliza, yameanzaje hadi mtu atumie mitandao ya kijamii amtukane kiongozi wa ngazi ya juu mwenye hadhi na heshima kubwa bila ya sababu yoyote.

Tunadhani muda umefika hasa kwa vijana kuitumia vyema mitandao hiyo kwa kujiongezea elimu na wasiitumie vyengine kwani wanachangai kuharibika kwa maadili.

Aidha wale wanaofurukutwa na siasa sio vyema kututukania viongozi wetu kwa sababu viongozi hao wamekuwa na heshima kubwa kwetu, lakini pia hawawatendei haki wanapowatukana bila sababu.

Ni wakati wa vyombo vya sheria kuwachukulia hatua wale wanaotumia vibaya mitando hiyo kwa kuharibu maadili yetu.