MOGADISHU, SOMALIA

TAARIFA kutoka nchini Somalia zinaeleza kuwa watu wachache wanajitokeza kupokea chanjo ya corona katika taifa hilo liliopo pembe ya Afrika.

Somalia ilipokea dozi 300,000 za chanjo ya Astra Zeneca ya virusi vya corona mwezi Machi lakini, maofisa wa afya wanasema chini ya nusu ya dozi hizo zimetumika.

Mamlaka inasema kasi ya polepole ya utoaji wa chanjo kunatokana na kufunga wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan na habari potofu kuhusu chanjo yenyewe.

Hospitali ya Banadir iliyopo mjini Mogadishu ni moja ya vituo vikuu vya chanjo katika mji mkuu wa Somalia.

Tangu kuanza kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani, watu wachache wamejitokeza kupata chanjo, ambayo ni muhimu katika mapambano dhidi ya janga la virusi vya corona duniani.

Dk. Ubah Farah mkurugenzi wa afya ya familia katika wizara ya afya nchini humo alisema sababu ambayo ilisababisha kasi ndogo ya chanjo ya COVID-19 ni kufunga katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Aidha alisema kuwa pia wapo watu wanasita kwenda kupata chanjo ya Astra Zeneca kutokana na kuwepo taarifa za chanjo hiyo kusababisha damu kuganda ka na dhana kwamba dawa hiyo inaweza kusababisha utasa.

Kiasi cha Wasomali 130,000 hadi sasa wamepatiwa chanjo, lakini dozi zilizobaki muda wake utakwisha baada ya miezi michache ikiwa hazitatumika.

Dk. Abdinassir Ibrahim Moalim ni mkurugenzi wa kituo cha kitaifa cha simu cha COVID-19 katika mji mkuu, Mogadishu, alisema wamepokea simu 18,000 kwa siku katika miezi miwili iliyopita.

Maofisa wanaandikisha viongozi wa dini ya kiislamu katika juhudi za kuwashawishi watu zaidi wachukue chanjo hiyo, mmoja wa walimu mashuhuri wa kidini katika taifa hilo, Sheikh Abdi-Hayi Sheikh Adam, alisema chanjo hiyo haiingilii Ramadhani.