NA HAJI NASSOR, PEMBA
MAKAMU wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Massoud Othman, amekemea tabia ya baadhi ya watumishi wa umma kutengenezea maneno mazuri na yenye kukubalika kwa mabosi wao kutokufanya kazi, bila ya kujuwa kuwa kufanya hivyo ni kudhoofisha kasi ya Rais wa sasa wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi.
Alisema, wapo watumishi wamekuwa wakipewa jukumu la kutekeleza wajibu wao, lakini hushindwa kulitekeleza na kisha kutengeneza maneno mazuri, ambayo kiakili yanakubalika.
Makamu huyo wa Kwanza, aliyasema hayo ukumbi wa Wizara ya Fedha Gombani Chake chake Pemba, alipokuwa akizungumza watumishi waliochini ya ofisi yake, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tano, kisiwani humo.
Alieleza kuwa, kwa uzoefu wake wa utumishi Serikalini na kwenye mashirika mengine ya kimataifa, amegundua kuwa waliowengi wamekuwa wakifikiria utungaji maneno mazuri ya kumpa bosi, huku jukumu alilopewa kutokamalika.
“Hii ndio kufanyakazi kwa mazowea, hebu sasa tubadilikeni, kwa kufuata kasi ya Dk. Mwinyi ya kuwatumikia wananchi wa Zanzibar lazima na sisi watumishi tuifuate kwa dhati,’’alieleza.
Hivyo Makamu huyo wa kwanza alisema, kuendelea kulemaa na utungaji wa maneno mazuri ya kutokufanyakazi kazi au kutokamilisha jukumu la mtumishi alilopangiwa, ni kulichelewesha taifa kufikia linakokusudia.
Katika hatua nyingine, Makamu huyo wa kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Massoud Othman, aliwakumbusha watumishi hao kuwa, ofisi yao ni nyeti na kubwa hivyo lazima wawe wabunifu wakati wanapowahudumia wananchi.
Alisema, kila mtumishi anawajibu wakulifanya jukumu la ofisi hiyo kama lake, ili sasa ajenge hamu na nidhamu kubwa ya kazi zake ambapo kufanya hivyo, ni kuitendea haki Katiba ya Zanzibar.
“Kila mmoja ni shahidi kuwa ofisi ya Makamu wa kwanza, imeanzishwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, sasa lazima tuiwajibikie ipasavyo,’’alieleza.
Aidha Makamu huyo wa kwanza, aliwahakikisha watumishi hao kuwa, atatetea na kuzilinda haki zao kama zilivyoanishwa kwenye sheria, kanuni na maazimio ya utumishi wa umma.
Mapema Katibu Mkuu wa ofisi hiyo, Khadija Khamis Rajab, alisema wameshajipanga kimkakati, ili kuhakikisha changamoto kadhaa kama za uharibifu wa mazingira wanazitatua.
Alieleza, sasa mfumo wao pamoja na kuendelea kutoa elimu, lakini wamejiongeza kwa kuweka miundombinu mfano ujenzi wa kuta za kuzuia mimong’onyoko.
Alifahamisha, mfano wa hayo ni eneo la Msuka wilaya ya Micheweni ambapo kunauharibifu mkubwa wa fukwe, unaosababishwa maji ya bahari kupanda juu, hivyo wazo la kujenga ukuta linakuja.
“Pamoja na kufanya hivyo, sasa tumeanzisha mpango wa uoteshaji miti aina ya mikoko katika eneo ambalo tutagundua kuna uharibifu mkubwa wa mazingira,’’alifafanua.
Hata hivyo Katibu Mkuu huyo, alimuhakikishia Makamu huyo wa kwanza kuwa, wazo lake la kutoa elimu kwa kutumia mitandao ya kijamii, watalifanyia kazi.
Makamu huyo wa kwanza wa Rais Zanzibarm Othman Massoud Othman, pamoja na ujumbe wake, upo kisiwani Pemba kwa ziara ya siku tano, ambapo pamoja na mambo mengine atawajulia hali wagonjwa kisiwani humo.