NA JUMBE ISMAILLY, IGUNGA

WATUMISHI watatu wa Mamlaka ya Maji na Usafii wa Mazingira Igunga (IGUWASA) wanashikiliwa na jeshi la polisi wilayani Igunga, Mkoani Tabora kwa tuhuma mbali mbali zikiwemo za ubadhirifu wa fedha ambazo bado kiasi chake kinafanyiwa uchunguzi zaidi ili kiweze kufahamika.

Wanaoshikiliwa na jeshi hilo, ni pamoja na ofisa wa kitengo cha biashara katika Mamlaka hiyo, Benedict Bayo (34), ofisa wa kitengo cha ufundi wa Iguwasa, Alex Julius (33) na msoma mita wa Mamlaka hiyo, Daniel Matandiko (31).

Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira, (IGUWASA) Wilaya ya Igunga, Hussein Salum Nyemba, alifafanua kwamba watumishi hao walikamatwa ikiwa ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na  kikao cha kamati ya ulinzi na usalama pamoja na kikao cha wadau wa maji kilichokaa katikati ya wiki iliyopita.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo aliweka bayana kuwa yeye binafsi baada ya kuhamia kikazi katika wilaya ya Igunga alikuta kuna changamoto nyingi za ubadhirifu katika Mamlaka hiyo, ikiwemo baadhi ya wananchi kwa kushirikiana na baadhi ya watumishi kushiriki katika wizi wa maji.

Alisisitiza Nyemba kwamba baada ya kubaini hali hiyo ndipo alipoanza kufanya uchunguzi na kubaini kuwa zaidi ya wateja 810 kwa miezi mitatu mita zao, zinasoma sifuri huku wakitumia maji na kwamba kila mwezi Iguwasa imekuwa ikipoteza maji kwa asilimia hamsini kutokana na hujuma mbali mbali.

Mkurugenzi huyo, alibaini pia kwamba baadhi ya magati hayajaingizwa kwenye mfumo huku baadhi ya fedha za makusanyo ya mauzo ya maji hayo yamekuwa yakitumiwa binafsi na afisa biashara wa maji, huku akiwa hajataja kiwango chake kwa kuhofia kupoteza ushahidi.

Aidha, Nyemba aliweka bayana kuwa kutokana na upotevu wa mapato hayo makubwa hivi sasa IGUWASA inadaiwa na KASHUWASA zaidi ya shilingi milioni 671 zilizosababishwa na baadhi ya watumishi wa mamlaka hiyo, akiwemo afisa biashara wa maji wa Iguwasa, Benedict Bayo.

Alisema kutokana na deni linalodaiwa na Kashuwasa, hivyo IGUWASA ipo hatarini kusitishiwa huduma ya maji endapo watakuwa hawajalipa fedha hizo  kabla ya mwisho wa mwezi huu.

Sambamba na hayo, vile vile, Mkurugenzi huyo wa IGUWASA alisema baada ya kuona hali hiyo alilazimika kuitisha kikao cha dharura kilichoongozwa na Mkuu wa wilaya ya Igunga, John Mwaipopo, kilichowahusisha viongozi wa dini.

Baadhi ya watumiaji wa maji, viongozi wa vyama vya siasa pamoja na kamati ya ulinzi na usalama na kufikia maamuzi ya kukamatwa kwa wote waliohusika na ubadhilifu wa fedha hizo na kuharibu mita ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wamekwishanunua pikipiki 10 zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 20 zitakazotumika kufuatilia wizi wa maji kwa wale wanaoharibu mita na kwamba hatakuwa na huruma kwa mtumishi yeyote yule atakayebainika kufanya hujuma kwenye vyanzo vya maji.

Mwenyekiti wa Chama cha U.D.P. ambaye pia ni msemaji wa vyama vya siasa wilayani Igunga, Mbogo Athumani alimpongeza Mkurugenzi huyo, kwa kubaini ubadhirifu huo wa fedha na kutoa wito kwa wananchi wa Igunga kuunga mkono juhudi za serikali kwa kuwafichua wezi wa maji.

Nao baadhi ya wananchi wa wilaya ya Igunga, Asia Juma, Aloni Jackson, Rehema Mussa pamoja na Sudi Abeid, walisema watamuunga mkono Mkurugenzi huyo kutokana na kazi kubwa aliyofanya kwa kipindi kifupi tangu alipofika wilayani Igunga na kutumia wasaa huo kumuomba Waziri wa Maji,Jumaa Aweso afike Igunga ili wampe ufisadi wa Iguwasa.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga, Lucas Bugota, alisema anasikitishwa na hujuma iliyofanywa na baadhi ya watumishi wa Iguwasa na hivyo kuwataka wabadilike katika kuachana na hujuma hizo.

Naye Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Igunga, Anuwari Kashaga alisema Chama Cha Mapinduzi hakiko tayari kuona baadhi ya watumishi wakihujumu mradi wa maji ambao serikali imetumia mabilioni ya fedha na hivyo kuiagiza serikali ya wilaya ya Igunga kuwasaka wote waliohusika na kuwafikisha Mahakamani.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi, Sofia Jongo, alithibitisha kushikiliwa kwa watumishi hao watatu wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (IGUWASA) na kuahidi kwamba wanaendelea na uchunguzi na pia wataendelea na operesheni ya kuwasaka wengine waliohusika.

Hata hivyo, Kamanda Jongo alitoa wito kwa watumishi pamoja na wananchi kuacha mara moja kujihusisha na vitendo vya uhalifu na badala yake wafanye kazi zenye kutambulika kisheria kwani bila hivyo hawatabaki salama.