NA MAULID YUSSUF, WEMA

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Simai Mohammed Said amewataka wanafunzi wa kidato cha sita kuhakikisha wanaachana na vitendo vya udanganyifu katika kipindi chote cha mitihani yao ya taifa.

Waziri huyo alieleza hayo wakati alipofanya ziara ya kuangalia maandalizi ya mitihani kwa wanafunzi wa kidato cha sita katika Skuli ya Aboud Jumbe Mwinyi iliyopo Fuoni mkoa wa Mjini Magharibi.

Alisema kuna siri nyingi za kupata ufaulu mzuri kwenye mitihani ya taifa, lakini kwenye siri hizo suala la udanganyifu halimo na badala yake matokeo mazuri yatapatikana kwa kusoma kwa bidii.

“Kupata ufaulu mzuri kunahitaji bidii katika masomo na sio kufanya udanganyifu, napenda sana niwaeleze kuwa acheni kabisa tabia ya udanganyifu haikusaidiini”, alisema waziri huyo.

Simai aliwasisitiza wanafunzi kuondosha hofu wakati wanapofanya mitihani yao na badala yake wajiamini na wasome vizuri na wayafahamu masuali wanayotakiwa kujibu katika mitihani hiyo.

Alisema serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia wizara ya Elimu, ipo karibu na wanafunzi hao ili kuhakikisha wanapata matumaini ya kufanya vizuri kwenye masomo yao.

Aidha alitoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanakua karibu na watoto wao ili kuwapa matumaini ya kufanya vizuri katika mitihani hiyo.

Simai alisema kuwa wanafunzi 2,749 kwa Zanzibar wanafanya mitihani ya taifa ya kidato cha sita ambapo wanawake ni 1,428 sawa na asilimia 51.94 na wanaume  ni 1,321 sawa na asilimia 48.05.

Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya Elimu Sekondari wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Asya Iddi Issa akizungumzia somo maalum la sanaa (fine art), alisema Idara yake inajivunia kuwa na darasa la pekee la kidato cha sita la somo hilo  kwa Tanzania nzima.

Mkurugenzi huyo alisema somo hilo  ambalo limeanza kufanyiwa mitihani mwaka huu linasomeshwa katika skuli ya Aboud Jumbe Mwinyi iliyopo Fuoni.

Alisema darasa hilo hukuza  kirahisi  sanaa ambapo  ameiomba jamii kwa yeyote mwenye uwezo wa kuwawezesha sanaa hiyo kwa kushirikiana na wanafunzi hao  kuhakikisha wanawashirikisha katika matukio mbalimbali ili waweze kuonyesha vipaji vyao.

Jumla ya vituo 38 vitatumika kufanya mitihani ikiwa Pemba ni vituo 10 na vituo 28 kwa Unguja kwa skuli za serikali na binafsi.