WIZARA ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Mohammed, amesema uundwaji wa majiji unategemea aina ya Halmashauri, Mabaraza ya miji au Manispaa zilizokuwepo kwenye jiji husika.

Alisema mfumo wa jiji la Zanzibar umezingatia zaidi uwezo wa Manispaa tatu ambazo zinaunda jiji ikiwemo  Manispaa ya Mjini, Manispaa ya Magharibi ‘A’ na Manispaa ya Magharibi ‘B’.

Kauli hiyo alitoa wakati akijibu suala la nyongeza liloulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini, Machano Othman Said, ambae alisema ni mwaka mmoja sasa katika kuanzishwa kwa jiji hilo na upande wa pili wa  Jamhuri wana mifumo tofauti ya jiji na hapa inaonesha wamefuata mfumo wa Dar es salam hivyo hawaoni kuwa mfumo wa Mwanza ni mzuri kuliko huo unaotumiwa.

Alisema kwa sasa wanaona huo ndio mfumo mzuri zaidi, kuliko kufuata mfumo mwengine ikiwemo majiji ya Tanzania bara hasa ukilinganisha katika vyanzo vya mapato na ukubwa wa maeneo.

Waziri Masoud, alikiri kuwa ni kweli mifumo inayotumiwa katika majiji ya mwanzo, Dodoma na Tanzania bara ni mizuri lakini inatokana mifumo yake.

Akizungumzia suala la bajeti ya jiji alisema uundwaji wa jiji hilo umeundwa mwaka 2019, baada ya upitishwaji wa bajeti hivyo kwa mwaka huu tayari jiji limetegewa bajeti yake ambayo itasomwa katika makadirio na mapato na matumizi ya bajeti ya wizara hiyo.