NA ASYA HASSAN
WIZARA ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi imeomba kuizinishiwa zaidi ya shilingi bilioni 19,117, 400,000 kwa ajili ya matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Waziri wa wizara hiyo Riziki Pembe Juma alisema hayo katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi alipokuwa akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka huo.
Alisema kupatikana kwa fedha hizo kutasaidia wizara hiyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa na kuleta tija hapa nchini.
Alisema wananchi wanahitaji huduma mbalimbali ndani ya wizara hiyo, hivyo kupatikana kwa fedha hizo zitasaidia kuendesha na kusimamia shughuli mbalimbali za kimaendeleo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wa Zanzibar na nje ya Zanzibar.
Alisema katika mwaka ujao fedha wizara hiyo inatarajia kuimarisha maeneo ya ardhi kwa ajili ya kutumiwa kwa makaazi na shughuli nyengine za kimaendeleo.
Kupitia hatua hiyo Riziki alisema wizara yake kupitia kamisheni ya ardhi imepanga kutayarisha hati za haki ya matumizi ya ardhi 1,900, mikataba 140 ya ukodishwaji ardhi na vitambulisho 100 vya matumizi ya ardhi ya eka tatu.
Alisema pia wanatarajia kuendeleza ukaguzi wa maeneo 150 ya uwekezaji na maeneo 150 ya eka tatu za ardhi ya kilimo pamoja na kufanya kazi za uthamini wa ardhi kwa maeneo 350 kwa ajili ya shughuli mbalimbali.
Mbali na hayo alisema wataendelea kuwatambua wenye haki ya matumizi ya ardhi kwa viwanja 2000 na kufanya uhakika wa maeneo ya ardhi 1500 Unguja na Pemba.
Alisema kufanikiwa kwa kazi hizo kutasaidia kutatua baadhi ya changamoto ziliyopo pamoja na kuleta tija katika matumizi ya maeneo hayo.
Akizungumzia kazi zitakazofanywa na bodi ya uhaulishaji wa ardhi katika kipindi hicho alisema ni pamoja na kutoa elimu ya uhaulishaji wa ardhi kwa wananchi na masheha katika shehia 12 pamoja na kusimamia uhaulishaji wa ardhi kwa kujadili na kupitisha maombi 1,500 ya uhaulishaji yatakayowasilishwa.
Akizungumzia Shirika la Nyumba alisema katika kipindi hichi Shirika hilo imejipanga kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo ikiwemo kuanza ujenzi wa jengo jipya la kibiashara na makaazi (G+5)-Kiembe Samaki pamoja na kuanza ujenzi wa majengo mapya ya Makaazi katika eneo la Kwa Mchina.
Akiwasilisha hotuba ya maoni ya kamati ya mawasiliano, ardhi na nishati kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo, mjumbe wa kamati hiyo Fatma Ramadhan Mohammed alisema kamati hiyo inasisitiza kuimarisha matumizi na umiliki halali wa ardhi ili kupunguza migogoro inayotokana na rasilimali hiyo.
Mjumbe huyo alisema hayo kwa niaba ya Mwenyekiti wa kamati hiyo Yahya Rashid Abdulla, alisema kamati hiyo imebaini kuna changamoto mbalimbali ambazo zinachangia mahakama ya ardhi kushindwa kutekeleza vyema majukumu yake na kutofikiwa kwa lengo la chombo hicho.
Akizitaja changamoto hizo alisema ni pamoja na uhaba wa fedha za matumizi, ukosefu wa vitendea kazi na uhaba wa mahakimu hali ambayo inasababisha kurudisha nyuma utekelezaji wa majukumu yake.
Mbali na hayo kamati hiyo imesisitiza ufatiliaji wa karibu kwa watu wanaopeleka maombi ya hati za ardhi kwa ajili ya makaazi na badala yake wanabadilisha matumizi hayo kwa kufanya matumizi ya kibiashara ikiwemo mahoteli na nyumba za kibiashara.