NA NASRA MANZI, WHVUM

WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita amewataka wanafunzi wa Chuo cha Afya Zanzibar kufuata misingi wanayofundishwa katika fani ya uuguzi ili kupatikana wataalamu watakaosaidia wananchi wenye matatizo ya afya.

Akizungumza na viongozi wa huduma za uuguzi kutoka hospitali ya Mnazi Mmoja pamoja na wanafunzi kutoka Chuo cha Afya ikiwa ni kilele cha siku ya wauguzi duniani, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa hospitali ya Mnazi Mmoja.

Waziri Tabia alisema muuguzi yoyote atakayetekeleza majukumu yake kwa misingi ya kitaaluma hatalalamikiwa na wagonjwa na wananchi wanokwenda kupatiwa huduma za afya.

Aliwataka wanafunzi hao kutovunjika moyo kwa kusoma na kufanya kazi kwa bidii katika fani ya uuguzi kwa kuonesha ari na mapenzi kwa kuipenda fani hiyo.

Aliwanasihi vijana hao kuwajibika katika nafasi zao ili kufikia azma ya serikali katika kuimarisha huduma za kiafya kwa wananchi.

Alisema Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo itaendelea kushirikiana na Wizara ya Afya ili kuona wagonjwa katika hospitali wanahudumiwa ipasavyo na kuwekewa mazingira safi.

Alitoa wito kwa Jumuiya nyengine kuiga mfano wa chuo hicho kwa kushirikiana na wauguzi katika kuwakagua wagonjwa na kujumuika  katika kuwasaidia suala la kufanya usafi katika hospitali  bila ya kusubiri siku ya maadhimisho.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji hospitali ya Mnazi Mmoja Dk. Msafiri Marijan alisema serikali ya awamu ya nane imekuwa na uwazi, umakini katika utendaji wa kazi ,hivyo ni vyema wanaoshughulikia masuala ya wagonjwa kutoa huduma nzuri kwa jamii pamoja na kuwajibika ili watu kupata huduma bora za kiafya.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la wauguzi na wakunga, Dk. Amina Abdulkadir Ali aliitaka jamii kutodharau fani ya uuguzi na ni vyema kuhamasika, kuipenda taaluma hiyo, pamoja na wakunga kutoachwa nyuma kwa kupewa kipaumbele katika utendaji wa majukumu yao.

Msaidizi Mkurugenzi huduma za uuguzi hospitali ya Mnazi Mmoja, Tatu Khamis Hussein aliwataka wafanyakazi wanaohusika na masuala ya uuguzi kutoa huduma nzuri na kufanya kazi kwa uadilifu na uweledi kwani wauguzi ni jambo kubwa lakini linahitaji umakini katika kuwapatia huduma wagonjwa.

Mkurugenzi Mtendaji Chuo cha Afya Aziza Hamid alisema jitihada zinafanyika katika kuwatengeneza na kuwafundisha wanafunzi hao ili kuwa viongozi bora wa baadae. Siku ya wauguzi duniani huadhimishwa kila ifikapo Mei 12 kila mwaka  duniani kote.