NA KHAMISUU ABDALLAH

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, imewasisitiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanafuata miongozo ya elimu hasa katika suala la kujipaka piko na mapambo mengine yasiyoendana na umri wao.

Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Mkurugenzi Maandalizi na Msingi wa wizara hiyo, Asya Iddi Issa, wakati akizungumza na Zanzibar Leo ofisini kwake Mazizini.

Alisema kinapofika kipindi cha sikukuu watoto wengi hasa wa msingi na sekondari wamekuwa wakikiuka muongozo kwa kupaka piko, kukata nywele kwa mikato isiyoendana na maadili na silka ya kizanzibari.

Kaimu Asya alisema ni marufuku kwa mwanafunzi yoyote kwenda na piko skuli kwani hiyo ni moja ya mapambo ambayo yamekatazwa kwa mujibu wa muongozo wa elimu Zanzibar.

Aidha alisema kwa mujibu wa muongozo namba 10 wa elimu umeeleza mambo mbalimbali yanayowahusu wanafunzi kufanya na kutofanya wanapokwenda skuli.

Alisema, muongozo huo umeelezea mambo mbalimbali ambayo hayatakiwi kwa wanafunzi ikiwemo kutovaa herini, sare za skuli zisishonwe za kubana na mambo mengine ambayo ni miongoni mwa mapambo.

Alisema zamani watoto walikuwa wakipakwa hina tupu katika kipindi cha sikukuu, lakini hivi sasa wazazi wamekuwa wakiyakuza kwa kuwapaka watoto wao piko jambo ambalo sio zuri.

“Zamani tulikuwa tunachorwa barabara tu unatiwa kidoto mkononi au herufi ya jina lako lakini hivi sasa utamuona mtoto wa darasa la kwanza, la pili na sekondari anajichora piko bila kujua kwamba anakwenda kinyume na miongozo ya elimu,” alisema.

Kaimu Asya, alisema piko ni moja ya mapambo na haikubaliki kwa mujibu wa muongozo wa elimu ya Zanzibar.

Hivyo aliwasisitiza wazazi na walezi kuwaepusha watoto wao kuvunja sheria za elimu hali ambayo inaweza kuwasababishia changamoto ikiwemo kurudishwa nyumbani na kukosa elimu.

Mbali na hayo, aliwaasa watoto wa sekondari kuachana na mambo ya kupita na kujikita katika kutafuta elimu ambayo itawasaidia baadae kuwa viongozi watakaolisaidia taifa lao kimaendeleo.

Nao baadhi ya wazazi na walezi walisema ni kweli hivi sasa utandawazi umebadilika hali ambayo watoto wanapakwa piko na hina hali ambayo sio maadili ya kizanzibari.

“Piko na hina hupakwa mtu pale anapoingia katika ndoa lakini wenyewe sasa hivi utasikia sayansi na teknolojia mpaka mtoto ndogo anapakwa piko na hina”, walisema.

Hivyo, waliwaomba wazazi kurudi katika mila, silka na utamaduni wao wa awali ambao mtoto alikuwa akipakwa hina tupu kwa ajili ya sunna kwa siku ya Edd el Fitri.