NA MARYAM HASSAN, TUWERA JUMA (MCC)

WIZARA ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto imesema itahakikisha inaimarisha huduma za mama na mtoto ili kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi, ikiwa ni moja ya kipaumbele chake katika mwaka huu wa fedha.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Wizara hiyo Nassor Ahmed Mazrui, wakati akiwasilisha makadirio na matumizi kwa mwaka wa Fedha 2021/2022 katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi.

Alisema watahakikisha upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi na afya ya mama na mtoto katika ngazi ya msingi sambamba na kuongeza vituo vya daraja la pili kwa ajjli ya kutoa huduma za kujifungua.

Alisema wizara ya Afya kwa mwaka huu wa fedha imezingatia maelekezo ya serikali ya awamu ya nane katika kuimarisha utoaji wa huduma ambapo wizara hiyo imejikita katika kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa katika matukio mbali mbali ya kitaifa.

Aidha alisema maamuzi ya serikali ya kurejesha huduma zilizogatuliwa katika sekta mama, wizara itahakikisha kwamba huduma hizo zitaendelea kuimarishwa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ya upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wote.

Aidha alisema katika vipaumbele vyengine vilivyowekwa na Wizara ni pamoja na kuimarisha uwezo wa utayari wa kupambana na maradhi ya miripuko na majanga ya kiafya, ambapo itaimarisha mifumo ya miundombinu ya kiafya ya kujiweka tayari katika udhibiti athari zitokanazo na majanga hayo.

Mazrui alisema wizara itasimamia utekelezaji wa sheria na taratibu zilizowekwa ikiwemo manunuzi pamoja na kuendeleza jitihada za kutokomeza ugonjwa wa malaria Zanzibar.

Sambamba na hayo alieleza kuwa wataimarisha huduma za upatikanaji wa dawa, vifaa vya utabibu na uchunguzi kwa kuimarisha huduma hizo kuwa zinapatikana katika ngazi zote.

Akiwasilisha hotuba ya maoni ya Ustawi wa Jamii kuhusiana na makadirio na mapato kwa mwaka wa Fedha 2021/2022 mjumbe wa kamati hiyo Abdalla Abass Wadi alisema kamati imebaini kuwa kupungua kwa baheri mwaka huu kutapelekea baadhi ya huduma kutolewa chini ya kiwango, ama kutopatikana kwa wakati husika.

Kamati hiyo imeshauri wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango ushirikiano na Wizara ya Afya kuangalia kwa makini hali ya kupungua kwa bajeti katika programu kuu ya uchunguzi na matibabu.

Kwa upande wa Mkemia Mkuu wa Serikali, alisema kamati haikupendezwa na taarifa ya kusambazwa kwa mchele ambao haukuwa na kiwango kwa ajili ya matumizi ya binadamu na baada ya miezi mitatu ndio hatua za kuuangamiza mchele huo kati ya tani 3000 zimechukuliwa.

“Kamati ilipohoji kwa wahusika wakuu imegundua kuwa bado tani 2950 ziko madukani, ambapo tayari nyengine zimeshatumiwa na binaadamu”,alisema mjumbe huyo.

Aidha alisema kujitokeza kwa suala hilo imebainika kuwa maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kufanya uzembe na kuacha kutekeleza wajibu wake wa kufanya kazin kwa ufanisi kwama sheria inavyoelekeza.

Kwa mujibu wa sheria ya Wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi namba 2 ya mwaka 2006 wao ndio wenye uwezo wa kisheria kupeleka sampuli iliyoleta mashaka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ilipogundulika.

Aidha alisema kamati imegundua kuwa umefanyika udanganyifu wa upelekaji wa sampuli ya mchele mwengine tofauti na mchele uliopo sokoni.

Kutokana na hali hiyo kamati inaiomba serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto kulichukulia hatua hali suala la uingizwaji wa bidhaa zilizokwisha muda wa matumizi na zisizokuwa na Kiwango, hali ambayo unapelekea athari kubwa kwa wananchi ikiwemo maradhi.

Kwa mujibu wa hutuba hiyo Wizara imeomba kuidhinishiwa jumla ya shilindi bilioni 197,868,5000,000 kwa ajili ya mishahara na shughuli za uendeshaji.