NA MWANDISHI WETU
VIGOGO, Yanga SC wameibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Mabao ya Yanga SC yamefungwa na mshambuliaji Mburkinabe, Yacouba Sogne dakika ya 27 na winga Mkongo, Tuisila Kisinda dakika ya 30.
Kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 61 baada ya kucheza mechi 29, ingawa inabaki nafasi ya pili ikizidiwa wastani wa mabao tu na mabingwa watetezi, Simba SC ambao pia wana mechi nne kiganjani, wakati JKT Tanzania inabaki na pointi zake 33 za mechi 30 katika nafasi ya 14.
Mechi nyingine ya ligi kuu , wenyeji Gwambina FC wamelazimishwa sare ya 0-0 na Namungo FC Uwanja wa Gwambina, Misungwi mkoani Mwanza.
Gwambina wanafikisha pointi 31 baada ya kucheza mechi 29 na kusogea nafasi ya 16 wakiizidi wastani wa mabao tu Ihefu SC, wakati Namungo imefikisha pointi 37 baada ya kucheza mechi 27, japo inabaki nafasi ya 10.
Ikumbukwe mwishoni mwa msimu timu nne kati ya 18 zinazoshiriki ligi kuu zitashuka moja kwa moja na mbili zitakwenda kucheza na timu za Daraja la Kwanza kuwania kubaki kwenye ligi hiyo.
@@@@@@@
3.
Mafunzo yajipanga kuvuna pointi
NA HASHIM KASSIM
KOCHA mkuu wa timu ya Mafunzo FC inayoshiriki ligi kuu soka Zanzibar Abdallah Mohamed (Edo), amesema maandalizi ya kujiandaa kukamilisha michezo iliyobaki katika ligi inaendelea vizuri.
Aliyasena hayo wakati wa mazoezi ya timu hiyo uwanja wa Matumbaku, yanayofanyika kila siku, licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya kutokuwa na wachezaji wote.
Edo alieleza kuwa wamelazimika kuanza mazoezi mapema ili waweze kutimiza malengo waliyojiwekea, ikiwemo ya kumaliza ligi katika nafasi tatu za juu.
“Malengo yetu ni kumaliza katika nafasi tatu za juu kwa sababu tunashindana, kwa kuwa hatuko kwenye ligi kwa kushiriki na lengo ni kutwaa kikombe, naimani wachezaji watakua vizuri baada ya muda mchache” alisema Edo.
Naye kipa namba moja wa timu hiyo Mwinyiureji Hassan alieleza kuwa wachezaji wana matumaini makubwa ya kufanya vizuri kutokana na maandalizi yao.
Ligi kuu soka Zanzibar inatarajia kuendelea kuanzia tarehe 22 mwezi huu katika viwanja mbalimbali Unguja na Pemba, huko.