NA ABDI SHAMNA, IKULU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuna umuhimu wa serikali kuwa na sera, ili kukiwezesha Chama cha Mabaharia Zanzibar (ZASU) kufanya kazi kwa taratibu na mfumo maalum.
Dk. Mwinyi alieleza hayo jana ikulu jijini Zanzibar, alipokutana na uongozi wa Chama cha Mabaharia Zanzibar (ZASU), ambapo alisema kuna umuhimu kwa serikali kuwa sera itakayokwendana na sheria ili kukiwezesha ZASU kufanya kazi kwa taratibu ikiwemo ushughulikiaji wa haki na utatuzi wa matatizo mbali mbali wanayopata mabaharia.
Alisema anakusudia kufanya kikao cha pamoja kitakachowahusisha wadau, wakiwemo viongozi wa Shirika la Meli, Shirika la Bandari na Mamlaka ya Usafiri Baharini (ZMA) ikiwa ni njia ya kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazokwaza uendeshaji wa Chama hicho.
Dk. Mwinyi alisema serikali itazifanyiakazi changamoto na mapendekezo yaliowasilishwa, ikiwemo ya kupata taasisi itakayoweza kuingiza fedha ili kukiwezesha chuo cha Mabahari kinachokusudiwa kujengwa nchini ili kijiendeshe.
Aidha, Dk. Mwinyi alikubali ombi la Uongozi wa Chama hicho la kuwa mlezi wa Chama cha Mabahari Zanzibar (ZASU).
Mapema, Katibu wa Chama cha Mabaharia Zanzibar (ZASU) Hussein Nassor Uki, alisema chama hicho kinakabiliwa na changamoto katika uendeshaji wa shughuli zake, ikiwemo ya kuitaka ZMA kuweka sharti kwa kampuni zinazosajili meli zake hapa nchini kutoa nafasi ya angalau mabaharia watano.
Alisema kuna umuhimu wa serikali kufikiria kuanzisha mafunzo ya muda mfupi, wakati huu ikiazimia kujenga Chuo maalum cha Mabaharia.
Aidha, alisema kuna haja kwa serikali kuangalia suala la mikataba na maslahi ya wafanyakazi wa vyombo vya ndani vya usafiri, vinavyofanya shughuli zake hapa nchini, hasa ikingatiwa wafanyakazi wa vyombo vyote na vile vinavyomilikiwa na Shirika la Meli, hawana mikataba.
“Lakini pia tumependekeza kwa ZMA wafanyakazi wa kima cha chini, walipwe angalau shilingi milioni moja kwa mwezi, hivi sasa baadhi ya kampuni zinawalipa shilingi 300,000/- tu”, alisema.
Alieleza kuwa wakati huu Zanzibar ikielekeza nguvu kuinua uchumi wake kupitia uchumi wa Buluu, kuna umuhimu wa kuanzisha Mahakama ya Mabaharia kama zilivyo nchi nyengine Duniani, ili kuwawezesha Mahabaria kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu ya kazi zao.
Aidha, aliiomba serikali kuangalia uwezekano wa wanachama wa ZASU kupata fursa ya kushiriki katika Bodi mbali mbali zinazoundwa na wadau wa Chama hicho, ikiwemo ZMA, Shirika la Bandari pamoja na Shirika la Meli, kama ilivyokuwa katika kipindi cha nyuma.
Alisema hatua hiyo itakiwezesha chama hicho kupata muunganiko na mashirika la Kimataifa, ikiwemo Shirika la wafanyakazi wa Usafiri Duniani.
Katibu Nassor alitumia fursa hiyo kumuomba Dk. Mwinyi kuwa mlezi wa ZASU, kama ilivyokuwa kwa Muasisi na Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Abeid Amani Karume.
Chama cha Mabaharia Zanzibar (ZASU) ni chama cha kwanza cha wafanyakazi kilichoanzishwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume mnamo Septemba 22, 1949, kupigania haki na maslahi ya Mabaharia nchini.