NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amezipongeza juhudi za serikali ya India za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za kiuchumi na kijamii

Dk. Mwinyi aliyasema hayo jana ikulu jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi Mdogo wa India anayefanyia kazi zake hapa Zanzibar Bhagwant Singh.

Alisema kuwa Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na India ambao umesababisha nchi hiyo kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza miradi yake ya maendeleo.

Alitumia fursa hiyo kuipongeza serikali ya India kwa kuiunga mkono Zanzibar katika sekta ya afya, elimu, maji, kilimo, biashara, huduma za jamii na uendelezaji wa rasilimali watu.

Aidha, aliipongeza azma ya serikali ya India ya ujenzi wa chuo cha amali huko kisiwani Pemba ambacho kitatoa mafunzo ya utalii na usarifu wa vyakula.

Alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kutimiza malengo ya serikali ya kukuza ajira kwa vijana pamoja na kuifanya Pemba kuwa ni sehemu maalum ya uekeza sambamba na kutoa mafunzo kwa vijana katika kuendeleza sekta maendeleo ikiwemo utalii.

Dk. Mwinyi pia, alizipongeza juhudi za serikali ya India za kuuunga mkono juhudi za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha huduma za maji safi na salama.

Alipongeza mashirikiano yaliopo kati ya Zanzibar na India katika kusaidia masuala tiba na kutoa nafasi za masomo kwa wanafunzi kutoka Zanzibar.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuzikaribisha kampuni nchini India kuzitumia fursa mbali mbali zilizopo hapa Zanzibar kwa kuja kuekeza.

Aliongeza kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatafuta namna bora ya kuzitumia hudumza mikopo zinazotolewa na India kwa ajili ya kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo hapa nchini.

Pamoja na hayo, Dk. Mwinyi alimuhakikishia Balozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya pande mbili hizo.

Mapema Balozi Mdogo wa India anayefanyia kazi zake Zanzibar Bhagwant Singh aliupongeza uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya India na Zanzibar na kusisitiza kwamba nchi yake itauendeleza kwa manufaa ya pande mbili hizo.

Balozi Singh alimpongeza Dk. Mwinyi kwa kasi kubwa ya maendeleo sambamba na azma yake ya kuipaisha Zanzibar kiuchumi na kuahidi kwamba India itaendelea kuziunga mkono juhudi hizo.

Aidha, Balozi Singh alieleza kwamba nchi yake itaendea kutoa nafasi za masomo kwa Zanzibar zikiwemo zile za muda mfupi kwa watendaji wa Serikali kupitia Mpango wa India Technical and Economic Cooperation Program” (ITEC) na “International Forestic Science’(IFS).

Pia, Balozi huyo alieleza hatua za nchi hiyo za kuendelea kusaidia upatikanaji wa vitendelea kazi na kuleta wakufunzi katika Chuo cha Amali  huko Vitongoji Pemba mradi ambao utawasaidia sana vijana katika kuwapatia mafunzo ya utalii na usafifu wa vyakula na hatimae kuwajengea soko la ajira.

 Balozi Singh alilipokea wazo la Dk. Mwinyi la kuwakaribisha wawekezaji wa sekta binafsi kutoka nchini India kuja kuekeza hapa Zanzibar na kuahidi kulifanyia kazi.