MADRID, Hispania

KLABU ya Real Madrid imethibitisha kujiuzulu, Zinedine Zidane kama kocha mkuu wa ‘Los Blancos’.
Real Madrid imeshindwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Hispania, ikizidiwa kwa tofauti ya pointi mbili dhidi ya majirani zao, Atletico Madrid.
“Zidane ameamua kuachia nafasi yake kama kocha mkuu wa klabu yetu, sasa ni wakati wa kuheshimu uamuzi wake na kumuonyesha shukrani zetu kwa weledi wake, kujitolea na mapenzi kwa miaka yote”.
Zidane mwenye umri wa miaka 48 ameifundisha Real Madrid katika vipindi viwili tofauti, awamu ya kwanza ilikuwa kati ya 2016 mpaka 2018, ambapo alikiongoza kikosi hicho kwenye michezo 149 na kushinda mataji tisa, ikiwemo ubingwa wa ‘La Liga’ na Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu mfululizo.
Na alirejea kwa mara ya pili Machi 11, 2019 mpaka Mei 27, 2021 na katika awamu hii amefanikiwa kushinda mataji mawili tu, ikiwemo ubingwa wa Hispania msimu uliopita, na amekiongoza katika michezo 114.(Goal).