ZASPOTI
KOCHA Mkuu wa Real Madrid, Zinedine Zidane, amethibitisha kuwa ataondoka klabuni hapo mara baada ya kumalizika kwa msimu huu hata kama atachukua ubingwa wa Ligi Kuu ya Hispania.

Kulingana na taarifa za vyombo vya habari vya Hispania, Madrid ambayo iliondokana na ushindi mbele Granada kwa kuifunga magoli 4-1 wakiwa ugenini, kwa sasa wapo katika nafasi ya pili ya msimamo wa ‘La Liga’ wakiwa na pointi 78 nyuma ya Atletico Madrid yenye pointi 80 huku michezo miwili ikisalia.

Zidane (48) akiwa Madrid ameshinda mataji mawili ya ‘La Liga’ na mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye misimu minne ambayo ameitumikia klabu hiyo, ameamua kuondoka baada ya mechi yao ya mwisho dhidi ya Villarreal itakayopigwa Mei 23 kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu.
Zidane huenda akawa chaguo la kwanza la Juventus na timu ya taifa ya Ufaransa iwapo watafanya mabadiliko ya kocha baada ya fainali za Euro 2021 zinazotarajiwa kuanza Juni 11.

Rais wa Real Madrid, Florentino Perez, yupo katika wakati mgumu kusaka mbadala wa Zidane ambapo inaelezwa anataka kumpandisha kocha Raul kuchukua mikoba ya ‘Zizzou’ ama atamchukua tena kocha, Max Allegri.
Zidane amesema anahisi hayuko kwenye moyo wa Perez na hata kama atachukua taji la ‘La Liga’ kwa mara ya tatu, rekodi ambayo atakuwa ameiweka ya kurudisha taji hilo kwa misimu miwili mfululizo.

Mfaransa huyo ameingia kwenye vichwa vya habari baada ya kutofautiana na mchezaji wake, beki kisiki Marcelo raia wa Brazil baada ya kumuacha katika kikosi chake kilichocheza na Granada huku ikielezwa kuwa wawili hao hawana uhusiano mzuri kwa sasa.
Marcelo atamaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu huu.

Beki huyo anasema Zidane amekuwa mtu wa kukosoa katika mazoezi wakati akizungumza na timu yake kuhusu ushindi wa mechi zake, lakini, pia alizungumza mbele ya meneja wa timu kuhusu kuamua kumuacha Marcelo na kumchukua kinda wa miaka 19, Miguel Gutierrez, kuanza.(AFP).