NA MWAJUMA JUMA

LIGI Daraja la pili wilaya ya Mjini hatua ya sita bora iliendelea juzi kwa kumalizia mzunguko wake wa pili kwa mchezo kati ya Amani Fresh na Maruhubi.

Mchezo huo ambao ulichezwa katika uwanja wa Mao Zedong ‘A’  saa 10:00 za jioni ulimalizika kwa wanaume hao kutoka sare ya kufungana bao 1 – 1.

Katika mchezo huo Maruhubi ndio waliotangulia kupata bao mnamo dakika ya tisa kupitia kwa mchezaji wake Mohamed Ali Abdalla bao ambalo lilidumu hadi mapumziko.

Miamba hiyo iliyokuwa ikishambuliana kwa zamu ilirudi katika kipindi cha pili na Amani Fresh kuongeza juhudi za ushambuliaji na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha bao hilo katika dakika ya 50 lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na Mohammed Salum Dadi.

Kuingia kwa bao hilo kulizidisha kasi ya mashambulizi kwa kilsa upande ambapo Maruhubi iliyoonekana kuliandama zaidi lango la wapinzanzi wao hao walipunguzwa kasi baada ya mchezaji wake Ramadhan Bakari kutolewa nje baada ya kuoneshwa kadi nyekundu .

Kwa matokeo hayo Amani Freshi imefikisha pointi nne sawa na Union Rangers wakati Maruhubi imefikisha pointi mbili sawa na timu za Danger na Negro FC huku Sebleni akiwa na pointi moja mkiani mwa ligi hiyo.