NA KHAMISUU ABDALLAH

ALIYEDAIWA kumdharau askari baada ya kumsimamisha barabarani kwa lengo la kupitisha msafara wa Makamu wa Pili wa Rais na kudharau, amefikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.

Abdalla Omar Ali (25) mkaazi wa Chumbuni, alifikishwa katika mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe mbele ya Hakimu Amina Mohammed Makame.

Mwendesha Mashitaka, Koplo wa Polisi Salum Ali, alidai mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Mei 10 mwaka huu.

Alidai siku hiyo, ikiwa ni majira ya saa 9:20 za alaasiri, mshitakiwa huyo alipatikana na kosa la kushindwa kusimama, wakati aliposimamishwa na askari wa Polisi akiwa katika majukumu yake ya kazi.

Alidai tukio hilo, lilitokea huko Mazizini Polisi wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, ambalo ni kosa chini ya kifungu cha 141 (1) (a) cha sheria namba 7 ya mwaka 2003 sheria za Zanzibar.

Ilifahamishwa kwamba, mshitakiwa huyo akiwa ni dereva wa gari yenye nambari za usajili Z 397 HX P/V akitokea upande wa Migombani kuelekea Kiembesamaki.

Alishindwa kusimama baada ya kusimamishwa na askari Polisi F 6175 akiwa amevaa sare za Polisi akiwa kazini, kwa ajili ya kupitisha msafara wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Mshitakiwa Abdalla, aliposomewa shitaka hilo alilikubali na kuiomba mahakama imsamehe huku upande wa mashitaka ukidai kuwa, hauna kumbukumbu ya makosa ya zamani kwa mshitakiwa huyo mahakamani hapo, hivyo adhabu itolewe kwa mujibu wa shitaka alilipatikana nalo.

Hakimu Amina, mara baada ya kumtia hatiani mshitakiwa huyo, alimtaka kulipa faini ya shilingi 20,000 na akishindwa atatumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa mwezi mmoja, ili iwe fundisho kwake na madereva wengine wanaodharau sheria za barabarani.

Mshitakiwa huyo alilipa faini hiyo ili kujinusuru kwenda jela kwa muda huo.